MCHEZO wa mieleka ni mchezo unaohitaji nguvu na huchezwa sehemu mbalimbali duniani kwa kanuni na sheria tofauti.
Ipo mieleka inayochezwa kisasa ambayo imeingiza
michezo mingine ya kupigana, lakini ipo mieleka ya asili ambayo
haihusishi aina nyingine za kupigana.
Kati ya michezo hiyo ya mieleka ya asili upo mchezo wa mieleka wa asili wa Senegal.
Mchezo wa mieleka nchini Senegal kwa asili
ulianzia kwa watu Serer, lakini baadaye mchezo huo ulikuwa maarufu na
kuwa mchezo wa taifa wa Senegal, pia katika nchi ya Gambia.
Kwa raia wa Senegal, mchezo huu wa mieleka wanauita kwa jina la kwao ambalo ni Laamb.
Kihistoria mchezo wa mieleka nchini Senegal
ulianzia kwa watu wa Serer ambao walikuwa wakiutumia kama sehemu ya
mazoezi kabla ya kwenda vitani, pia ulikuwa ikitumiwa na wavuvi baada ya
kazi zao, lakini baadaye mchezo huu ukawa unatumiwa na vijana
kuonyeshana uwezo wao wa nguvu, kupata wake, kuthibitisha uanaume wao au
kuleta heshima kijijini, ambapo mvuto wake ukaufanya kuwa mchezo wa
mashindano.
Katika karne ya 14 baada ya mchezo huo kuwa wa
kimashindano, aliibuka bingwa Boukar Djilak Faye kutoka kwa watu wa
Serer ambaye alishinda mapambano mengi na kuwa mtu maaarufu katika nchi
za Senegal na Gambia.
Tangu miaka ya 1950 mchezo huu wa mieleka ya asili
nchini Senegal ulikuwa kwa kasi zaidi kimashindano na kupata watazamaji
wengi na kuwa kivutio cha utamaduni kwani pia zawadi za fedha zilianza
kutumika katika kipindi hiki.
Hivi sasa mchezo huu nchini Senegal unaendeshwa
kibiashara na mapromota ambao wanatoa zawadi za fedha nyingi kwa
washindi na ushindani wake umekuwa mkubwa zaidi.
Kutokana na hali hiyo, wacheza mieleka nchini
Senegal wanafanya sana mazoezi tofauti, magumu kwa ajili ya kujiongezea
nguvu, pia wacheza mieleka hao wanatumia madawa ya kienyeji kabla ya
mapambano yao wakiwa na imani yanawaongezea nafasi zaidi ya ushindi.
Mabingwa wa mieleka wanaofahamika sana nchini
Senegal ni Yekini (Yakhya Diop), Tyson (Mohamed Ndao) na Bombardier
(Serigne Ousmane Dia).
Mapromota wa mchezo wa mieleka nchini Senegal
wanautangaza mchezo huu na wadhamini wamejiingiza sana kiasi kwamba yapo
mapambano mjini Dakar ambayo bingwa huchukua kitita za dola 120,000 au
zaidi ya hapo kwani wapo mapromota ambao hutumia kiasi cha dola 400,000
kuandaa pambano moja kubwa.
No comments:
Post a Comment