WAKATI
Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Pili ukianza leo nchini kote, Serikali
imesema kuanzia sasa, mtihani huo utakuwa ni wa mchujo kuanzia sasa,
hivyo atakayefeli atatimuliwa.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa(pichani) alisema mtihani wa mwaka
huu, matokeo yake yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato
cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa
alama 30.
"Mtihani wa kidato cha
pili kama ilivyo mitihani mingine ya taifa ni muhimu sana. Matokeo ya
mtihani huu hutumiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kama
sehemu ya matokeo katika mtihani wa taifa wa elimu ya sekondari kidato
cha nne," alisema Dk Kawambwa.
Alisema mtahiniwa
ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa
atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi
aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Dk Kawambwa alisema
kurudishwa kwa mchujo katika mtihani huo ni moja ya njiia ya kuboresha
elimu nchini na kupata wanafunzi walio bora nchini.
Alisema hayo ni mabadiliko ya kawaida na yataendelea kuwapo katika sekta hiyo kila mwaka
"Tunachopambania hapa
ni ubora wa elimu nchini na hii itasaidia kuondoa wanafunzi
wanaosemekana wanamaliza shule hawajui kusoma, japokuwa mimi siamini
kama ni kweli," alisema Dk Kawambwa.
Alisema mtihani huo
utamalizika Novemba 16, mwaka huu na idadi ya shule na vituo
vilivyosajili watahiniwa mwaka huu ni 4,242 ikiwa ni ongezeko la vituo
55 ikilinganishwa na vile vilivyosajiliwa mwaka 2011 ambavyo vilikuwa
4,187.
"Kwa hiyo kwa mwaka huu kuna ongezeko la asilimia 1.3," alisema Dk Kawambwa
Alisema watahiniwa
442,925 wamejiandikisha kufanya mtihani. Kati yao wasichana ni 214,325
(sawa na asilimia 48.39) na wavulana ni 228,600 (sawa na asilimia
51.61).
"Wizara inaagiza wadau
wote wa elimu katika kanda, manispaa na halmashauri za wilaya pamoja na
wazazi kuhakikisha kuwa wanafunzi wote walioandikishwa kufanya mtihani
wanafanya bila kukosa," alisema Dk Kawambwa.
Januari mwaka huu Serikali iliamua kurudisha mtihani huo kwa lengo la kupunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kuwa uamuzi wa Serikali wa
kurudisha mtihani huo, umezingatia vigezo katika kuboresha matokeo ya
kidato cha nne.
Mulugo alisema kuwa kuwapo kwa mtihani huo kutapunguza idadi ya wanaoshindwa kufaulu kidato cha nne.
“Kumekuwa na wanafunzi
wazembe ambao wamefanya kupungua kwa idadi ya ufaulu kutokana na
kukosekana kwa mtihani wa kidato cha pili, ambao ndiyo mwongozo wa
mwanafunzi kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali,” alisema Mulugo.
Chanzo - Mwananchi
0 comments:
Post a Comment