Mcheza sinema maarufu wa Kimarekani,
Angelina Jolie, ametangaza kwamba amefanyiwa operesheni ya kuondosha
matiti yake yote mawili ili kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya
maziwa na ya kizazi.
Kwa mujibu wa makala yake
iliyochapishwa leo kwenye gazeti la The New York Times na kupewa jina
"Chaguo langu la kitabibu", Angelina Jolie amesema ameamua kutangaza
jambo hilo hadharani ili kuwapa moyo wanawake wengine wenye historia ya
familia zinazouguwa saratani.
Mama yake mwenyewe Angelina alifariki
akiwa na miaka 56 kutokana na maradhi hayo. Sasa muigizaji huyo maarufu
wa sinema duniani, anasema anawataka wanawake wenye hali kama yake
kutafuta ushauri wa kitabibu na kufanya uamuzi baada ya kuwa na taarifa
za kutosha ili waweze kuendelea kufanya kazi, kama alivyofanya yeye.
"Licha ya kuweza kulifanikisha hili
na kubakia kimya kwa muda mrefu, sasa naandika kulitangaza kwa sababu
natarajia kuwa wanawake wengine wanaweza kufaidika na uzoefu wangu."
Ameandika mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya masuala ya
wakimbizi.
Uamuzi mgumu lakini muhimu
Jolie aliamua kufikia uamuzi huo wa
kuyaondosha matiti yake yote mawili, kwa sababu alifahamishwa na
madaktari wake kwamba alikuwa na chembechembe inayoongeza hatari ya
kupata saratani kwenye maziwa yote mawili na kwenye fuko lake la uzazi.
Kutokana na chembechembe hiyo iitwayo
BRCA1, madaktari walikisia kwamba alikuwa kwenye kiwango cha asilimia
87 ya hatari ya kupata saratani ya maziwa na asilmia 50 ya kupata
saratani ya kizazi.
"Baada tu kujua kwamba huo ndio
ukweli kuhusu hali yangu, niliamua kuchukua hatua za kabla na angalau
kupunguza kiwango hicho cha hatari kadiri nilivyoweza. Nikafanya uamuzi
wa kuondosha matiti yangu yote mawili. Nilianza na maziwa kwa kuwa
saratani ya maziwa ni kubwa zaidi kuliko hatari ya ile ya fuko la uzazi,
na operesheni ya fuko la uzazi ni kubwa zaidi," ameandika Jolie.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 37
amesema kwamba tarehe 27 Aprili alikamilisha miezi mitatu ya taratibu
za kitabibu kuhusiana na operesheni hiyo ya kuondosha matiti na kwamba
sasa kiwango cha uwezekano wa kupata saratani kimepungua hadi asilimia
tano.
Jolie na mumewe, ambaye pia ni
muigizaji maarufu, Brad Pitt, wana watoto watatu wa kuwazaa na watatu wa
kuwalea, na ameandika kwamba sasa anaweza kuwaambia watoto wake kwamba
hawapaswi kuwa na hofu ya kumpoteza mama yao kwa sababu ya saratani.
0 comments:
Post a Comment