Miongoni
mwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo wasanii wa hip hop nchini ni
kuingiza fedha kutokana na kazi zao. Bahati mbaya njia pekee na za
uhakika za kuingiza fedha kupitia muziki zilizobakia ni malipo ya show
na yale yanayotokana na miito ya simu.
Ni miaka takriban mitano sasa hakuna tena usambazaji wa albam
unaoaminika kama ule wa zamani kwakuwa wasambaji wa muziki wanaonekana
kuususia muziki wa Bongo Flava.
Kwakuwa shows na miito ya simu ndio njia pekee zilizobakia kumuingiza
fedha msanii wa Tanzania, inahitajika kazi ya ziada kutengeneza nyimbo
zinazoweza kuwavutia wadau wanaohusika.
Kwa miaka mingi, wasanii wanaofaidika zaidi ni wale wanaoimba (Ali
Kiba, Diamond, Dully Sykes, Ommy Dimpoz na wengine). Watu wengi
wameendelea kuamini kuwa Hip hop ni muziki wa kupata heshima tu Tanzania
lakini haulipi.
Chukulia mfano wasanii wenye sifa kubwa za kiuandishi kama Nikki
Mbishi, One the Incredible, Nash MC na wengi wa aina hiyo kwenye kizazi
chao. Rappers hawa licha ya kukubalika kwa uwezo wao usio na kifani,
muziki wao umeendelea kubaki kuwapa heshima tu lakini usiowaingizia
fedha inayostahili. Lakini hali hii ni tofauti kwa Roma na Nay wa
Mitego.
Roma
Jina la Roma lilianza kufahamika kwenye wimbo Mr President
na kumtambulisha rapper huyo kwa identity yake ya rap ya ‘kupayuka’ na
kama rapper mwenye mrengo wa kimapinduzi zaidi ‘radical rapper.’ Kwa
lugha nyingine rahisi, Roma alionekana kama mwanaharakati.
Roma alijitengenezea upekee wake kama rapper anayeukosoa vikali
uongozi wa serikali ya chama cha mapinzuzi, CCM. Licha ya Mr President
kuwa wimbo wenye style na beat ‘ngumu’ maudhui yake yaliufanya uwe
rahisi kuyakuna masikio ya mashabiki yaliyotaka kusikia anachonena.
Uwasilishaji wenye Kiswahili rahisi na maneno yanayoeleweka moja kwa
moja ni sababu nyingine iliyoupa uhai wimbo huu.
Baadhi ya nyimbo zake zilipata wakati mgumu kupata airtime kwenye
vituo vingine vya radio. Baada ya Mr President, Roma aliendelea kutoa
nyimbo zenye muelekeo ule ule ukiwemo Pastor
uliokuwa ukizungumzia jinsi dini inavyotumika kibiashara na pia
Mathematics ambamo alizungumza mengi na kuikosoa serikali na watu
binafsi.
Ingawa alikuwa ameshanza kupata mashavu, Mathematics ndio wimbo uliompa mafanikio zaidi.
Mwaka 2011 na mwishoni mwa 2012, Mathematics ilikuwa ni hip hop
anthem kwenye kila radio nchini. Umaarufu wa Roma uliongezeka maradufu.
Ukubwa wa Mathematics ulidhihirika wazi kwenye tuzo za Kili kwa kuwa
wimbo bora wa Hip Hop mwaka 2012.
Pamoja na kufanya hip hop ngumu, Roma amekuwa akipata mashavu kibao
ya shows. Ni miongoni mwa wasanii wachache wa hip hop Tanzania
wanaojulikana kwa kupiga show nyingi za promotion za makampuni
mbalimbali nchi nzima.
Hizi ni baadhi ya sababu zilizomfanya Roma awe msanii wa hip hop wa biashara:
1.Ni kuegemea kwenye utunzi wa nyimbo za kimapinduzi zinazowagusa
wananchi wengi hususan vijana waliochoka na jinsi hali ya kiuchumi
ilivyo nchini
2. Mashairi yake kuendana na hali halisi ya maisha ya mtaani
3.Ujasiri wake wa kusema mambo kwa uwazi bila kuogopa wahusika
anaowataja kwenye nyimbo zake. Ama kwa maana nyingine Roma husema mambo
ambayo wengine huogopa kuyasema.
4. Uwezo wake mkubwa wa kulitawala jukwaa wakati wa kuperform kitu
kinachosaidiwa na rap yake ya kupayuka ambayo ni nzuri kwenye live
performance.
5. Uandishi wa maishari ya kiubunifu yanayoeleweka kwa urahisi.
Hatumii sana metaphors kama wana hip hop wengine. Hii ni kwakuwa
mashabiki wa kawaida hawapendi kuumiza kichwa kujaribu kuelewa mistari
ya wimbo). Pia amekuwa akiepuka matumizi ya mistari ya Kiingereza.
6. Ile hali ya kuonekana kama mwanaharakati.
Nay wa Mitego
Kumekuwepo na mjadala mrefu kuhusiana na kama Nay wa Mitego ni
mwanahip hop ama anafanya Bongo Flavour (kwa kuzingatia neno bongo flava
linavyotafsiriwa na wengi kama muziki wa kuimba zaidi).
Wadau wengi wa hip hop licha ya Nay kujiweka kama msanii wa hip hop,
wanadai kuwa hafanyi hip hop. Mjadala huo tunawaachia mashabiki
wanaosikiliza nyimbo zake.
Kama Roma, Nay alianza kwa kujitengeneza kama msanii asiyeogopa
kukosoa ama kuponda jambo analohisi haliko sawa. Tofauti na Roma, Nay
hakuongelea siasa. Yeye alideal na maisha binafsi ya wasanii wenzie.
Kama unakumbuka kwenye Itafahamika, Nay aliwadiss wasanii wengi waliopoteza umaarufu, wakiwemo Inspekta Haroun, Sister P, Rah P, Dudu Baya, P-Funk na wengine.
Aina hiyo ya muziki wake ilimtengenezea maadui wengi hasa wasanii
aliowaponda pamoja na mashabiki wao, lakini pia akaanza kujipatia
mashabiki wake waliyemuona ni mtu asiyekopesha (asiyeogopa kuongea
ukweli).
Mwanzo Nay alichukuliwa kama rapper anayetumia njia ya kudiss wenzie
ili kupata ‘cheap publicity’ ama njia ya kupata umaarufu wa haraka. Japo
ni ngumu kuthibitisha kama hiyo ndio ilikuwa dhamira yake, Nay
ameendelea kuwa msanii wa aina hiyo hiyo. Nyimbo zake nyingi za rap
zimekuwa na ujumbe unaoendana na zinazozua mjadala.
Breakthrough yake kibiashara ilichangiwa na ngoma yake ‘Nasema Nao’.
Humo aliwadiss watu wengi zaidi. Kauli yake kuwa wasichana wengi wa
Bongo Movies ni machangudoa iliwafanya waigizaji wengi wa tasnia hiyo
kumuijia juu. Kutokana na wimbo huo, Nay alipata interview nyingi kwenye
vituo vya radio na TV vilivyotaka kupata ufafanuzi zaidi wa kile
alichokisema. Kuhusu suala la wasanii wa kike wa bongo movie, aliendelea
kushikilia msimamo wake na kutoa mifano halisi ya waigizaji
aliowashuhudia wakifanya uchangudoa.
Aina ya nyimbo zake, zikamtengenezea mashabiki lukuki nchini.
Mwaka jana alikuwa miongoni mwa wasanii waliozunguka nchi nzima
kwenye show za Fiesta. Na huko mara nyingi alikuwa kati ya wana hip hop
waliopata shangwe nyingi zaidi. Miaka ya 2012 na 2013 imekuwa na
mafanikio makubwa kibiashara kwake. Amefanikiwa kupiga show nyingi
zikiwemo za matamasha makubwa na zile za promotion za makampuni hususan
ya simu. Nay ameendelea kupata mashavu kwenye promotion zote za Tigo,
Vodacom na Airtel ambazo zimemuingizia fedha nyingi.
Mwaka huu amefanikiwa kutengeneza hit single, Muziki Gani aliyomshirikisha Diamond na ambao umemweka kwenye sehemu nzuri zaidi kibiashara.
Hizi ni baadhi ya sababu zilizomfanya Nay awe msanii wa biashara:
1. Kurap masuala ya ukweli yanayowahusu wananchi wengi bila kukwepesha
2. Kukosoa wasanii wanaofanya mambo yasiyopendeza
3. Kuandika mashairi yenye utata (controversial lyrics)
4. Kuandika mashairi rahisi yanayoeleweka kwa urahisi
5. Uwezo wake wa kubadilika kwendana na soko
6. Ujasiri wake na uwezo wake wa kusimama kwenye kile anachokiamini
Uchambuzi umefanywa na Fredrick Bundala (Bongo5 Head of Content).Twitter: @skywizz
0 comments:
Post a Comment