Blogger Widgets

Tuesday, December 4, 2012

EWURA YAFUNGUKA YATANGAZA BEI YA MAFUTA TENA

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU BEI KIKOMO ZA MAFUTA AINA YA PETROLI KUANZIA
JUMATANO, TAREHE 5 DISEMBA 2012
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inatangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli hapa nchini. Bei hizi zitaanza kutumika kuanzia Jumatano, Tarehe 5 Disemba 2012. Pamoja na kutambua bei kikomo za bidhaa mbalimbali za petroli nchi nzima, ni muhimu kuzingatia yafuatayo.
(a) Bei za jumla na rejareja kwa mafuta aina zote ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa zimeongezeka ikilinganishwa na toleo lililopita la tarehe 07 Novemba 2012. 
Katika toleo hili, bei za rejareja kwa Petroli na Dizeli zimeongezeka kwa viwango vifuatavyo: Petroli Sh 70/lita sawa na asilimia 3.4; Dizeli Sh 10/lita sawa na asilimia 0.53. 
Bei ya Mafuta ya Taa imepungua kwa Sh 3/lita sawa na asilimia 0.1. Bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili zimeongezeka kama ifuatavyo: Petroli kwa Sh 69.56/lita sawa na asilimia 3.52; Dizeli kwa Sh 10.04/lita sawa na asilimia 0.52. 
Bei ya Mafuta ya Taa imepungua kwa Sh 3/lita sawa na asilimia 0.15. Mabadiliko haya ya bei yametokana na ongezeko la bei ya mafuta katika soko la dunia na kushuka kidogo kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani.
(b) Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta.
(c) Kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ilimradi bei hizo ziko chini ya bei kikomo (price cap) kama ilivyokokotolewa na fomula mpya iliyopitishwa na EWURA na ambayo ilichapwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 454 la tarehe 23 Desemba 2011.
(d) Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
 Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika.
(e) Wanunuzi wanashauriwa kuhakikisha kuwa wanapata stakabadhi ya malipo inayoonesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita. Stakabadhi hiyo ya malipo itatumika kama kidhibiti cha mnunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo; ama endapo utakuwa umeuziwa mafuta yenye kiwango cha ubora kisichofaa.

0 comments:

Post a Comment