Blogger Widgets

Wednesday, December 19, 2012

Mitambo ya Digitali sasa kuzimwa kwa hatua


MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imesema ifikapo Desemba 31 mwaka huu, haitazima mitambo yote ya analojia kwenda dijitali na badala yake, itazima mitambo hiyo katika mikoa kadhaa nchini.

Imesema imechukua uamuzi huo kwa kuzingatia kuwa maeneo mengi nchini, hayajafikiwa na huduma ya digitali na kwamba inatoa nafasi katika maeneo hayo, ili kufikia hatua hiyo kwanza.

Akihojiwa kupitia kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC1 hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma (pichani), alisema si sahihi kuzima mitambo hiyo kwa nchi nzima.

“Mikoa tutakayozima ni ile iliyoenea mfumo wa analojia tu, hatuwezi kuzima mahali ambako hata hiyo analojia haijaenea sana, tutakuwa hatujatenda haki,”alisema Profesa Nkoma.

Mkurugenzi huyo alisema hatua ya kuzima mitambo inahusu maeneo yote nchini, lakini kwa mpangilio kulingana ongezeko la huduma ya digitali katika eneo husika.

Pia akizungumza katika warsha ya kujadili changamoto na fursa zake jijini Dar es Salaam, iliyowakutanisha wadau wa utangazaji, Profesa Nkoma alisema kuanza kwa mfumo huo, kutasaidia kurahisisha matangazo .

Alisema Desemba 31 mwaka huu, itakuwa mwisho wa kutumia mfumo wa analojia katika meneo yote yaliyoanza kutumia mfumo wa digitali.

Aliitaja mikoa ambayo mfumo wa dijitali umefika kuwa ni Mwanza, Mbeya, Tanga, Dodoma, Arusha, Moshi na Dar es Salaam.

“Tutaanza na mikoa hii wakati mikoa mingine ikiwa inaendelea kufikiwa na mfumo huu kwani tusipokuwa makini tunaweza kuuharibu mfumo huu,” alisema Profesa Nkoma.

Mbali na hilo TCRA imewataka wananchi kuhakikisha wananunua ving’amuzi ili kuepuka usumbufu utakaojitokeza mara baada ya kuzimwa kwa mitambo hiyo.

0 comments:

Post a Comment