Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Shaif Hamad
akizungumza na wahanga wa vurugu za uchaguzi mdogo wa Bububu huko ofisi
kuu ya Chama hicho Mtendeni.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Maalim Seif Shaif Hamad
akizungumza na wahanga wa vurugu za uchaguzi mdogo wa Bububu (hawapo
pichani) huko ofisi kuu ya Chama hicho Mtendeni.
Mbunge wa Jimbo la Mtoni (CUF) Mhe. Faki Haji Makame akizungumza kwa
niaba ya waganga wa vurugu za uchaguzi mdogo wa Bububu, mbele ya Katibu
Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad (kushoto). Picha na Salmin
Said-Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar.
Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad amelaani kitendo cha vyombo vya dola kuwapiga
na kuwakamata wafuasi wa chama hicho na kuwaacha wa vyama vyengine na
askari waliojeruhi raia wasio na hatia, siku ya uchaguzi mdogo wa jimbo
la Bububu Septemba 16 mwaka huu.
Akizungumza na wahanga wa tukio hilo huko Makao Makuu ya CUF Mtendeni
mjini Zanzibar jana, Maalim Seif alikiita kitendo cha askari hao kuwa ni
cha kibaguzi kinachoweza kuathiri hali ya maelewano inayoendelea kudumu
Zanzibar.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, alisema
jukumu la vyombo vya dola ni kusimamia haki kwa raia na si kuwabagua,
kama walivyofanya wakati wa uchaguzi mdogo wa Bububu, ambapo wafuasi wa
CUF peke yao ndio waliopigwa na kukamatwa, wakati viongozi na wanachama
wa vyama vyengine walihusika wazi wazi katika vurugu hizo.
“Bila shaka huu ulikuwa mpango wa kupangwa, wanachama wa vyama vyengine
hawakuchukuliwa hatua yoyote, hata Mbunge hakuheshimiwa na alipigwa kwa
sababu tu anatoka CUF”, alisema Maalim Seif.
Alieleza kuwa katika mazingira ya amani na maelewano yaliyopo Zanzibar
haikutarajiwa baadhi ya viongozi wa serikali na wa CCM kusimamia askari
wa vyombo vya dola, wakiwemo walioficha nyuso zao kwa kuvaa ninja
kuwapiga na kuwakamata wananchi wasiokuwa na makosa kwa njia ya
kibaguzi.
Katika vurugu hizo wafuasi 22 wa CUF akiwemo Mbunge wa CUF jimbo la
Mtoni, Faki Haji Makame walikamatwa na wengine kujeruhiwa vibaya, katika
harakati za uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu, ambapo mgombea
Uwakilishi wa CCM alitangazwa kuibuka mshindi.
Wakati huo huo, Mbunge wa jimbo la Mtoni Faki Haji Makame amemshitaki
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai na askari Polisi wa
kituo cha Bububu kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Said Mwema.
Mbunge huyo analalamikia vitendo vya vya uonevu alivyofanyiwa wakati wa
harakati za uchaguzi mdogo wa Bububu na baadaye kubambikiziwa kesi.
Katika barua yake kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar ya Septemba 19,
ambayo nakala zake zilitumwa kwa Mkuu wa Polisi na Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano, Mbunge huyo alisema Vuai alishirikiana na vijana
wa CCM waliokuwa wamewekwa tawi la CCM Bububu na baadhi ya Polisi
kumwita kihadaa kumpiga na baadaye kumfungulia mashitaka.
“Wakati nikienda kuwatembelea jamaa zangu kule Bububu, Naibu Katibu Mkuu
wa CCM Zanzibar aliniita, nilipofika akawaleta vijana wa CCM wakanipiga
ngwara na nilipowaita Polisi walikuja kunichukua na kunifungulia
mashitaka ya kupigana hadharani”alilalamika Mbunge Makame.
Hata hivyo alisema anashangazwa na kitendo cha Polisi kuwaacha vijana
hapo pamoja na Vuai walioshiriki kumpiga na sasa hajui anashitakiwa
kupigana na nani.
Katika barua hiyo aliyoituma jana, alieleza kuwa vijana hao baadhi yao
walikuwa na vipande kadhaa vya kupigia kura waliachiwa na Polisi kupotea
na wala hawana kesi wakati yeye na wafuasi wengine wa CUF waliteswa na
kufunguliwa kesi.
Mbunge huyo anamtaka Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Zanzibar kuchunguza kwa
kina tukio hilo, kufuatia malalamiko ambayo tayari ameshayawasilisha
huku akiendelea na taratibu za kuwasiliana na wanasheria wake kusimamia
kesi hiyo.
Mbunge huyo alieleza kuwa ana wasiwasi askari Polisi Zanzibar
wanashirikiana na viongozi na wafuasi wa CCM kukiuka taratibu za kazi
zao za kusimamia haki kwa raia wote.
Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad leo
anatarajiwa kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa CUF huko katika
viwanja vya Kwa Geji Bububu, ikiwa ni mkutano wa kwanza tokea kufanyika
uchaguzi huo mdogo.
Maalim Seif alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Marekani na Uingereza,
wakati uchaguzi huo ulipofanyika, kufuatia kifo cha aliyekuwa
Mwakilishi wa jimbo hilo, marehemu Salum Amour Mtondoo.
Na
YUSHA SHABANI
Of isi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar
0 comments:
Post a Comment