Kufuatia
Utabiri wa Hali ya Hewa uliofanywa kwa pamoja na Mamlaka za Hali ya
Hewa kwa nchi za Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki, Mamlaka ya Hali ya
Hewa – Tanzania imetoa taarifa kuhusu uwezekano wa nchi kupata mvua
nyingi iliyo juu ya wastani. Hali hii ya kuwa na mvua nyingi inatabiriwa
kuikumba nchi kwa kipindi cha Oktoba, 2012 hadi Disemba, 2012 na huenda
ikaendelea zaidi.
Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya
Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga). Mvua zinatarajiwa
kuanza katika wiki ya tatu ya mwezi Septemba, 2012 katika mkoa wa Kagera
na kaskazini mwa Kigoma na kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza,
Shinyanga, Mara, Geita na Simiyu katika wiki ya nne ya mwezi Septemba,
2012. Kwa ujumla mvua hizo zinatarajiwa kuwa juu ya wastani katika
maeneo ya Kanda ya Ziwa Viktoria.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini
(Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na
Visiwa vya Unguja na Pemba): Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya
kwanza ya mwezi wa Oktoba, 2012. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani
hadi juu ya wastani katika maeneo mengi.
Nyanda za juu Kaskazini Mashariki
(Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara). Mvua katika maeneo haya
zinatarajiwa kuanza katika wiki ya pili ya mwezi Oktoba, 2012 na
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani.
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa).
Mvua zinatarajiwa kuanza katika
wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2012 katika mkoa wa Kigoma na wiki ya pili
ya mwezi Novemba katika mikoa ya Tabora, Rukwa na Katavi. Mvua
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mikoa ya Rukwa
na Kigoma. Aidha maeneo mengi ya mikoa ya Katavi na Tabora mvua
zinatarajiwa kuwa juu ya wastani.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na
Dodoma). Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Novemba
na zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani.
Nyanda za juu Kusini Magharibi
(Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro): Mvua
zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Novemba 2012 na
zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika mkoa wa Njombe
na kusini mwa mikoa ya Mbeya na Morogoro. Maeneo ya kaskazini mwa mikoa
ya Mbeya na Iringa, mvua zinatarajiwa kuwa juu ya wastani.
Maeneo ya Kusini na Pwani ya
Kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara): Mvua zinatarajiwa kuanza wiki
ya nne ya mwezi Novemba, 2012 na zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu
ya wastani katika maeneo mengi.
Kwa kuzingatia hali hii Ofisi ya
Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa tayari imetoa
taarifa/elimu kwa umma kupitia kipindi cha “Tuambie” cha TBC 1 na
kuelekeza taasisi na wadau mbalimbali kuchukua hatua za tahadhari. Mfumo
wetu wa kukabiliana na maafa una Kamati za Maafa kwenye ngazi ya mkoa,
wilaya hadi kijiji ambazo zina majukumu ya kusimamia masuala ya maafa
katika maeneo yao. Kamati zilizoanishwa hapo juu pamoja na wadau wote
mnakumbushwa kujiandaa kukabiliana na maafa endapo yatatokea. Katika
Jitihada za kujiandaa mnakumbushwa kuzingatia yafuatayo:-
1. Kutekeleza mipango mbadala
katika maeneo mliyobaini kuwa yana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na
mafuriko; kama vile kuhamisha wananchi maeneo ya mabonde kwenda sehemu
salama na kurejesha mawasiliano endapo yataharibika.
2. Kupatikana dawa muhimu za
magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na madawa ya kusafisha maji ya
kunywa (Water Guard Tablets).
3. Kupatikana kwa dawa muhimu za
mifugo kwani magonjwa miguu na midomo (FMD) na homa ya bonde la ufa
(RVF) yana uwezekano mkubwa wa kutokea.
4. Upatikanaji wa chakula cha kutosha. Aidha wananchi wahimizwe kuweka akiba ya chakula cha kutosha.
5. Kutenga fedha za kukabiliana na maafa endapo yatatokea.
6. Elimu kwa Umma itolewe kwa kuhusisha vyombo vyote vya mawasiliano na uongozi wa Vijiji na Mitaa.
7. Kuchukua hatua za ziada kwa maeneo ambayo yana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na mmomonyoko wa ardhi.
8. Kuainisha mitaro inayoweza kuingiza maji katika migodi ya wachimbaji wadogowadogo, na kuchukua tahadhari zinazostahili.
9. Kuhakikisha kuwa mifereji na mitaro ya maji machafu kwa maeneo ya Jiji/miji iko safi na wazi wakati wote kupitisha maji.
10. Kuchimba au kukamilisha uchimbaji wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua.
11. Maofisa Ugani – Kilimo kutoa
ushauri kwa wakati kuhusu mazao ya kupanda na pia wafugaji kutumia
nafasi kuvuna malisho ya kutosha yatakayotumika kipindi cha kiangazi .
12. Kila ngazi kujiweka tayari
kukabiliana na mafuriko ni muhimu kuunda timu za wataalam wa kukabiliana
na athari zitakazotokea, majina yao yaainishwe na waelekezwe cha
kufanya pindi hali ikiwa hivyo.
Ni matumaini yangu kuwa
tukishirikiana katika kukabiliana na mvua nyingi pamoja na majanga
yanayoambatana na mvua hizi, tunayo nafasi kubwa ya kujihakikishia
usalama wa nchi yetu kutokana na majanga ya asili.
Nashukuru kwa ushirikiano wenu.
IMETOLEWA NA KATIBU MKUU, OFISI YA WAZIRI MKUU
0 comments:
Post a Comment