WAKATI
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikitangaza kusudio lake la kukata rufaa
dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, iliyotengua ubunge wa
aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Dk. Dalali Kafumu, wadau mbalimbali
wameipongeza hukumu hiyo wakiita ni darasa tosha kwa demokrasia ya mfumo
wa vyama vingi.
Miongoni
mwa waliosifu hukumu hiyo ni pamoja na Spika mstaafu, ambaye pia ni
Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akisema kuwa
maamuzi hayo inafaa yaheshimiwe.
Akizungumza
jana mjini Tabora, Sitta alisema kuwa mahakama ina mamlaka yake
kisheria, hivyo wana CCM hawana budi kuyaheshimu maamuzi hayo kwani
imefanya kazi yake inavyotakiwa.
“Kama
kuna mtu anaona hukumu hiyo haikutenda haki, anaweza kwenda mahakamani
kukata rufaa, lakini mimi nashauri ni vema tujipange upya tuingie
ulingoni.
“Hapa
mimi sina maoni juu ya jambo hilo, bali cha msingi ni vema tukakaa na
kutafakari yaliyotokea huko Igunga, ili basi tukiona inafaa kukata rufaa
sawa, na kama tuingie ulingoni, yote ni sawa,” alisisitiza Sitta.
Katika
hukumu yake juzi, Jaji Mary Nsimbo Shangali, aliyekuwa akisikiliza kesi
hiyo, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA, Joseph
Kashindye, alisema kuwa alipokea malalamiko 15 ambayo yaliridhiwa na
pande zote mbili, lakini yakaongezwa madai mengine mawili na kufikia 17.
Mbali
na Dk. Kafumu, washitakiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali
pamoja na Msimamizi wa uchaguzi jimboni humo, Protace Magayane na kwamba
mahakama hiyo ilithibitisha madai saba ya kutengua matokeo hayo.
Hata
hivyo, wakati Sitta akiwa na mtazamo huo, CCM kupitia kwa Katibu wake
wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ilieleza
kutoridhishwa na hukumu hiyo, hivyo kuamua kukata rufaa.
Pamoja
na CCM kuchukua hatua hiyo, wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa na
wanaharakati waliliambia Tanzania Daima kuwa, hukumu hiyo ni darasa
tosha la demokrasia linaloonesha jinsi sheria za uchaguzi zinavyovunjwa.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashir Ali, alisema hukumu hizo
za uchaguzi ikiwamo hiyo ya Igunga, zina maana sana kwa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, wanasiasa na wananchi.
“Tatizo
letu huwa hatusomi hukumu hizi kwa undani, kwani tungekwishajua kuwa ni
darasa tosha la demokrasia. Suala la takrima lilikuwa halieleweki kama
ni rushwa, ushindani wetu wa kisiasa si wa kuvumiliana, una matumizi
makubwa ya fedha, mali za serikali na madaraka kwenye kampeni,” alisema.
Ali
alifafanua kuwa hukumu hiyo imetoa mwanga kuwa, kama hakuna chombo huru
cha kusimamia sheria zinazokiukwa ni sawa na bure, akitolea mfano Tume
ya Taifa ya Uchaguzi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa licha
ya kuwapo wakati wa mchakato huo, vilishindwa kuchukua hatua.
“Kuna
mjadala kuhusu uwepo wa sheria ya Tume ya Uchaguzi, maana tangu kuanza
kwa mfumo wa vyama vingi hakuna sheria ya Tume ya Uchaguzi, badala yake
chombo hiki kinatambuliwa na sheria za uchaguzi, jambo linalotoa mwanya
kwa mapungufu yanayojitokeza sasa,” alisema.
Kuhusu
uwajibikaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakati wa uchaguzi
huo mdogo, Ali alisema kuwa mpaka sasa umuhimu wa ofisi hiyo hauonekani
maana kama hoja ni kusajili vyama, kazi hiyo inaweza kufanywa hata
mahakamani.
Alibainisha
kuwa, kwa sasa ofisi ya msajili na Tume ya Uchaguzi ni kama idara tu
ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hivyo wananchi wanapaswa kutumia hukumu
ya Igunga kama tathmini wakati huu wa mchakato wa katiba mpya
kusahihisha makosa ya kuvifanya vyombo hivyo huru.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Mtatiro Julius,
alisema hukumu hiyo itawafungua wananchi kuona umuhimu wa kubadilisha
mfumo wa uchaguzi ili kuepusha taifa kuingia gharama zisizokuwa za
lazima pale kiongozi anapokufa ama kuenguliwa.
“Hii
naiona kama hatufikirii sawa sawa, maana matumizi ya mabilioni ya fedha
kwenye uchaguzi yalikuwa kwa vyama vyote kule Igunga hasa CCM, CHADEMA
na CUF. Lakini hili linaweza kuepukwa mana kama upuuzi unafanywa na watu
wawili, hatuna sababu ya kulisababishia taifa hasara,” alisema.
Kwa
mujibu wa Mtatiro, inapotokea hali kama hiyo ya mbunge kuenguliwa au
kupoteza maisha, mshindi wa pili kutoka chama kingine ndiye achukue
nafasi badala ya kurudia uchaguzi.
“Igunga
tuliona Dk. Kafumu walipishana kidogo na Kashindye wa CHADEMA, hivyo
kwa vile huyu alikiuka taratibu, basi mshindi wa pili apewe nafasi
kuliko kurudia uchaguzi, kwani kufanya hivyo kunaweza kukipa chama
kilichoenguliwa ushindi tena wa mtu asiyefaa,” alisema Mtatiro.
Mwanasiasa
huyo pia hakusita kuinyoshea kidole Ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa, akisema kuwa, John Tendwa (msajili) ameonesha wazi ni wakala wa
CCM anayefanya mbinu za kukisaidia chama hicho kishinde badala ya
kusimamia kanuni na sheria.
Mtatiro
aliweka bayana kuwa makosa yaliyoainishwa kwenye hukumu iliyomtia
hatiani Dk. Kafumu na kumnyang’anya ubunge wake, yalilalamikiwa mapema
na wapinzani kwa Msajili wa Vyama wakati wa kampeni, lakini hakuchukua
hatua yoyote.
“Msajili
wa vyama hana meno, na huyu amekuwa na kashfa ya kusajili hata vyama
visivyo na sifa ilimradi tu aweze kuvidhoofisha vyama makini vya
upinzani. Hata kwenye uchaguzi ameonesha wazi anataka CCM ishinde,”
alisema.
Mtatiro
aliongeza kuwa, umefika wakati nafasi hizo nyeti za vyombo kama Tume ya
Uchaguzi, Msajili na nyinginezo zitangazwe ili watu wenye taaluma zao
washindanishwe na kuchujwa na chombo maalumu badala ya kuteuliwa na
rais.
Naye
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea
Nkya, alizungumzia hukumu hiyo ya Igunga akisema imetoa tafsiri mpya kwa
wananchi kuelewa demokrasia ya vyama vingi na namna ya kumpata
mwakilishi makini bila rushwa na vitisho.
“Hili
litakuwa fundisho kwa wanasiasa wanaochezea fedha nyingi kwenye
uchaguzi kununua watu, maana watatambua sasa kuwa kufanya hivyo
kutawapotezea viti vyao. Lakini na wagombea wanapaswa kuwa makini na
wapiga debe na vyama vyao, kwani wanaweza kuingizwa mtegoni kama
alivyoponzwa Dk. Kafumu,” alisema.
Akisoma
hoja zilizothibitishwa na mahakama hiyo juzi, Jaji Shangali alisema ni
pamoja na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, kutumia nafasi yake ya
uwaziri kutoa ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo lilikuwa ni moja
ya kero kubwa kwa wananchi wa Igunga.Waziri Magufuli akiwa katika
uchaguzi mdogo huo katika moja ya kampeni, alitumia nafasi ya uwaziri
kuwatisha wapiga kura wa jimbo hilo kuwa kama hawatamchagua mgombea wa
CCM watawekwa ndani.
Jaji
Shangali pia alisema kuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage, alipita
mitaani akitangazia wananchi kuwa mgombea wa CHADEMA amejitoa.
Katika
hoja nyingine ni kwamba Imamu Swalekh Mohamed wa Mskiti wa Ijumaa
Igunga, aliwatangazia waumini wa Kiislamu kuwa wasiichague CHADEMA kwa
kuwa baadhi ya viongozi wake walimdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga,
Fatuma Kimario.
Nayo
matamshi ya Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, kudai kuwa CHADEMA
imeleta makomandoo kuuvuruga uchaguzi huo ni mojawapo ya hoja ambazo
mahakama hiyo ilizikubali.
Katika
hoja kuu ya mahindi, Jaji Shangali alihoji kama wananchi wa Igunga
walikuwa na njaa sana. Na kwamba, kama jibu ni ndiyo, ni kwanini
uchaguzi usifanyike wakati hawana njaa.
Chanzo: http://wotepamo
0 comments:
Post a Comment