Serikali imesema inafikiria kuifumua na kuivunja Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa kuwa imeshindwa kukidhi matarajio ya serikali pamoja na Watanzania wengi kama ilivyotarajiwa wakati inaanzishwa.
Bodi hiyo licha ya kupewa zaidi ya Sh. trilioni moja tangu ilipoanzishwa
mwaka 2005 hadi sasa, lakini imeshindwa kuweka mkazo ili kuhakikisha
inawabana watu wote waliopata mikopo walipe madeni yao ili fedha hizo
zitumike kuwakopesha wanafunzi wengine wanaozihitaji.
Aidha, kwa kipindi kirefu utendaji wa bodi hiyo umekuwa hauendi sawa
sawa na kumekuwa na malalamiko mengi katika utoaji wa mikopo katika vyuo
vikuu.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine
Gesimba, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam mbele ya Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
“Kwa sasa idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo hapa nchini kwa ajili ya
elimu ya juu ni 300,000, lakini hali ipo hivi sasa huko tuendako idadi
hiyo ikifikia 500,000 na kuendelea itakuwaje?” Alihoji Gesimba.
Aliambia kamati hiyo kuwa mpaka sasa HESLB imekusanya Sh. bilioni 20
kati ya Sh. bilioni 39 ambazo zinatakiwa kukusanywa na kwamba hayo ni
mapungufu makubwa ya kiutendaji.
Gesimba alisema kwa sasa kuna vyuo 50 vya elimu ya juu ambavyo
vinahudumiwa na HESLB na kwamba kila mwaka mahitaji yanazidi
kuongezeka.
Hata hivyo, Gesimba alisema bajeti ya elimu ya juu inazidi kupungua
ingawa idadi ya wahitaji inaongezeka kila mwaka na kwamba hiyo ni moja
ya changamoto zinazoikali wizara yake.
Alisema serikali imempa kazi mshauri mwelekezi kwa ajili ya kufanya
utafiti kuhusu matatizo katika utoaji wa mikopo na changamoto zake ili
aweze kuishauri wizara.
Aliongeza kuwa mtalaamu aliyepewa kazi hiyo tayari amemkabidhi rasimu
Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, na kwamba mpango mzima
ukikamilika serikali itapata njia sahihi ya utoaji wa elimu ya juu
nchini.
“Huyu mtalaamu atatuambia namna ya kupata vyanzo vya mapato
vitakavyosaidia wanafunzi kusoma, namna ya kukusanya mikopo kutoka kwa
wanafunzi walimaliza vyuo ambapo walipa mikopo pamoja na utendaji mzima,
lakini hayo yakifanyika bodi hii haiwezi kuendelea kuwepo tena,”
alisema.
Akizungumzia sekta ya elimu kwa ujumla, Gesima alisema serikali
inatarajia kuongeza ada kwa wanafunzi wanaosoma ualimu ngazi ya cheti
kutoka Sh. 150,000 hadi Sh. 200,000 kwa mwaka pamoja na kuanza kutoza
ada kwa ajili ya usajili wa shule binafsi za msingi na sekondari.
Alisema kwa sasa hakuna gharama yoyote inayotozwa mtu ama taasisi
binafsi inapotaka kusajili shule ya msingi pamoja na sekondari na
kuongeza kuwa ada ya ukaguzi kwa shule hizo nayo inatarajia kupanda
kutoka Sh. 500 kwa mwanafunzi mmoja hadi Sh. 1,000 kwa mwanafunzi.
Kuhusu ubora wa ufaulu, Gesima aliesema hakuna uhusiano wa moja kwa moja
na shule husika kufanyiwa ukaguzi mara kwa mara na kwamba takwimu
zianonyesha shule zilizoshika nafasi 10 za mwisho ndizo zilizokaguliwa
mara nyingi na kwamba zilizoshika nafasi 10 za kwanza zilikaguliwa mara
chache.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, alisema wizara hiyo
imepata hati chafu ya hesabu zake na kwamba kuna haja ya serikali
kujipanga ili kurekebisha dosari hizo wakati mwingine.
Alisema ni jambo la kusikitisha mpaka sasa wizara haina mfumo wa
kompyuta kutambua idadi ya walimu wake na madai mbalimbali wanayoidai
(Database) na kwama hatua hiyo inachangia matatizo mbalimbali katika
sekta ya elimu kuendelea kuwepo.
Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo, Gesimba alikiri kwamba Database ni muhimu na kwamba wizara itaanzisha utaratibu huo.
POAC YAIJUA JUU MUHIMBILI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) imeijia juu
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa kushindwa kutunza mali zake
pamoja na utunzaji mbovu wa taarifa za wagonjwa hususani mafaili na
majibu ya vipimo.
Kufuatia utendaji huo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Zitto
Kabwe, imeagiza hospitali hiyo kufunga ofisi za Benki ya NMB zilizopo
eneo la Muhimbili kwenye kiwanja cha hospitali kwa kuwa kodi ya pango
haiingii Muhimbili.
Wabunge wa kamati hiyo walifikia uamuzi huo kwa kueleza kwamba mwaka
2007/2008, POAC iliiagiza Muhimbili kurejesha eneo hilo mikononi mwake
badala ya kuendelea kushikiliwa na mbia ambaye ni Regent Store.
Inadaiwa kwamba mwaka 1987 Muhimbili na Regent Store, waliingia mkataba
wa ukodishaji wa eneo hilo ambao ulipaswa kumalizika baada ya miaka
mitano tangu kusainiwa yaani mwaka 1992.
Badala yake, Regent Store ilidai kwamba mkataba wao wa miaka mitano
ulitakiwa kuhesabiwa kuanzia mwaka 1992 ambao hata hivyo, ungeisha mwaka
1997 lakini haujasitishwa hadi sasa.
Kutokana na mkanganyiko huo, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola,
alieleza kushangazwa na ukimya wa Muhimbili hata baada ya kutoa muda
mrefu kwa mkodishaji kinyume cha mkataba.
Alisema baada ya mwaka 1997, Muhimbili walipaswa kumnyang’anya eneo,
lakini cha kushangaza walikaa kimya hadi mwaka 2005 ambapo Regent Store
ilikimbilia mahakamani kutaka ufafanuzi wa mkataba.
Hata hivyo, Mwanasheria wa Muhimbili, Veronica Hellar, alisema kesi
iliyopo mahakamani haihusiani na uhalali wa umiliki bali ufafanuzi wa
mkataba na kwamba inaendelea vizuri.
Alisema kesi hiyo namba 53/2005 imepangwa kusikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Desemba 3, mwaka huu na hukumu itatolewa.
Hata hivyo, Lugola alisema kesi hiyo haihusiani na agizo la kamati
ambalo linaitaka Muhimbili kufunga ofisi za NMB kwa kuwa benki hiyo
imekodishiwa pango kinyemela na inahesabika kama mvamizi.
Kwa upande wake, Zitto alisema kukodishwa kwa jengo hilo huku Muhimbili
ikikosa kodi ni kuikosesha hospitali dola za Marekani 7,200 kwa mwezi
kiasi ambacho kilithibitishwa pia na Mkurugenzi wa Fedha wa Muhimbili,
Agnes Kuhenga.
Baada ya maelezo ya wabunge, Zitto aliitaka Muhimbili kufunga ofisi za
NMB leo na kama haitafanya hivyo kamati yake itaenda kufunga ofisi hizo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Muhimbili, Profesa Joseph Kuzilwa,
aliiomba kamati kuahirisha agizo lake hadi Desemba 5, hukumu
itakapotolewa, lakini POAC ilikataa.
Profesa Kuzilwa na Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili, Dk. Marina Njelekela, walikubali kupokea agizo hilo na kuahidi kulifanyiakazi.
Awali, POAC ilibaini kuwepo kwa utunzaji mbovu wa kumbukumbu za taarifa
za wagonjwa hususani mafaili na kuchelewa kupatikana kwa majibu ya
vipimo.
Lugola alisema inashangaza kwamba kuna wagonjwa wanasubiri faili lao kwa miezi sita na hata majibu inakuwa hivyo hivyo.
Alisema jambo hilo ni hatari kwa kuwa wapo wanaopoteza maisha kwa sababu
tu faili halionekani au majibu yanachelewa huku akionya kuwa
inawezekana kuna mgomo baridi usiokwisha kwenye hospitali hiyo.
Akijibu, Dk. Njelekela alithibitisha kuwepo kwa tatizo la upotevu wa
mafaili ya wagonjwa na kwamba wameanza kulifanyiakazi kwa kuingiza
taarifa za wagonjwa kwenye mfumo wa kompyuta ambao unahitaji Sh. milioni
790.
Hata hivyo, alisema hospitali inakabiliwa na tatizo kubwa la fedha na
hivyo kwa sasa wanatafuta ufadhili wa wadau mbalimbali ili kutekeleza
azma hiyo.
Kutokana na maelezo hayo, Zitto alisema: “Mafanya nini Muhimbili maana
hata kazi ya kutunza kumbukumbu za wagonjwa hamuwezi, hivi hili nalo
mnasubiri wafadhili wafanye? Kwa nini zisitoke kwenye fedha zenu za
ndani?”
Akijibu, Dk. Njelekela alisema suala hilo litafanyiwa kazi na kwamba
linahitaji kila daktari awe na kompyuta yake na pia katika kila wodi.
Zitto aliagiza fedha hizo zipatikane mara moja na kwamba Muhimbili
iandike maombi ya fedha kwa Hazina na kutaka nakala ya barua hiyo
ipelekwe kwa POAC kwa ufuatiliaji.
Katika hatua nyingine, POAC imekosoa mfumo wa uagizaji wa dawa
unaofanywa na Muhimbili kwenda Bohari ya Dawa (MSD) na kueleza kwamba
una mwanya mkubwa wa wizi wa dawa za serikali.
Kamati hiyo imeeleza kwamba ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG) ya mwaka 2010/11 ilibaini kwamba Muhimbili imekuwa
ikiagiza dawa lakini baadhi yake zinapofika hospitalini hapo hazilingani
na zile zilizoagizwa.
Wajumbe wa POAC walieleza kuwa dawa au vifaa tiba ambazo hukataliwa na
Muhimbili vinakuwa vimelipiwa lakini hurudishwa MSD na kwamba katika
utaratibu huo kunatokea mwanya wa wizi.
Kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imeahidi kukutana na MSD pamoja na Muhimbili ili kuona namna ya kutatua tatizo hilo.
0 comments:
Post a Comment