Kauli ya TFDA, iliungwa mkono na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
iliyoweka wazi kuwa haitambui mbegu za ubuyu kuwa zinatoa mafuta ya
tiba, isipokuwa inatambua tiba inayotokana na mti huo ni majani, magome
na unga.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Mbadala wa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk Paulo Mhame, alisema Serikali haitambui mafuta ya
ubuyu kama tiba.
Hata hivyo, mwanzoni mwa wiki hii, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ilitangaza kuwa mafuta hayo ni salama yakitumiwa vizuri.
Daktari Bingwa wa Udhibiti wa Saratani wa taasisi hiyo, Dk Crispin
Kahesa, alinukuliwa akisema hadi sasa hakuna utafiti wowote wa
kitaalamu, uliopata kufanywa na kuonesha kuwa mafuta hayo ni chanzo cha
saratani ya ini.
“Mafuta ya ubuyu si dawa bali yanazuia maradhi sugu yasiyoambukiza,
ikiwamo saratani kwa sababu kitaalamu yana ‘anti oxidant’ (uchachu)
ambayo pia hupatikana kwenye baadhi ya matunda kama maembe, machungwa na
mananasi.
“Tofauti iliyopo, ni kwamba mafuta hayo yana anti oxidant nyingi
tofauti na iliyomo kwenye matunda. Anti oxidant husaidia kukinga maradhi
ambayo mengi si ya kuambukiza - maradhi sugu kama vile saratani,
kisukari na shinikizo la damu,” alikaririwa Dk Kahesa.
Kazi nyingine ya anti oxidant mwilini ilitajwa kuwa ni kuondoa sumu na kusaidia kutengeneza chembechembe hai mwilini.
“Narudia, mafuta ya ubuyu hayana madhara yakitumika vizuri, bali
madhara ambayo watu wanayasema, yanatokana na jinsi wanavyoyatumia,
kwani wajasiriamali wanaoyatoa hawajui ni mgonjwa gani anapaswa
kuyatumia na kwa wakati gani,” alikaririwa Dk Kahesa.
Kutokana na tamko hilo, wiki hii pia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Seif Rashid, jana alitangaza kuwa mafuta hayo si salama na
kusisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Serikali, hivyo wananchi waamue
kuyatumia au kutoyatumia.
Dk Rashid alitoa kauli hiyo kujibu maswali ya waandishi wa habari
baada ya kufungua semina ya siku mbili, iliyoandaliwa na TFDA na
Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Tayari chombo cha Serikali ambacho kina mamlaka juu ya hili
kimeshatoa tamko, hivyo ni hiari ya wananchi kuamua kuyatumia au kuacha.
“Kwa sababu ni sawa na sigara, tumesema kabisa sigara inasababisha
saratani na matatizo mengine, tukaweka na onyo kwenye kasha la sigara,
hivyo ni hiari kutumia au kutotumia,” alisema.