Wanafunzi
117 wa Polisi, wamefukuzwa katika Chuo cha Taaluma na Mafunzo ya Polisi
(MPA), kilichopo Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Waliotupiwa virago na kufutwa kwenye
kozi hiyo ni wale waliopoteza sifa za kuendelea na mafunzo ya kijeshi
baada ya kukutwa na makosa ya utovu wa nidhamu, utoro na matatizo ya
kiafya.
Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP),
Matanga Mbushi, ambaye ni mkuu wa chuo hicho alisema katika mahojiano
maalumu kwamba, waliotimuliwa chuoni ni kati ya askari wanafunzi 3,189
waliokuwa wamesajiliwa kuanza mafunzo ya kijeshi katika chuo hicho,
Oktoba 25 mwaka jana.
Kati yao askari 115 ni wale wa Polisi na askari wawili wanatoka
katika Idara ya Uhamiaji iliyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kufukuzwa kwa wanafunzi hao , kuna akisi moja kwa moja jinsi
menejimenti ya chuo hicho ilivyojipanga upya kupunguza wimbi la baadhi
ya askari walioko kazini na ambao wanalipaka matope jeshi hilo kutokana
na kupotoka kimaadili kwa kutaka kujinufaisha kimaslahi.
Askari hao walikuwa waungane na wenzao ambao wanatarajiwa kuhitimu
mafunzo ya awali ya polisi na uhamiaji, Julai 26 mwaka huu baada ya
kupatiwa mafunzo ya medani za kivita. Mgeni wa heshima atakayeshuhudia
kuagwa kwa askari 3,092 ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk.
Emmanuel Nchimbi.
Kamishna Mbushi alisema askari hao
pamoja na mambo mengine wamepatiwa mafunzo maalumu ya utunzaji wa amani
ya nchi iliyopo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Haki za
Binadamu, Masuala ya mtambuka (Cross cutting issues), Usimamizi wa
majanga na Usimamizi wa kazi za Polisi.
Mafunzo mengine ni pamoja na Polisi
Jamii, Sheria ya ushahidi, Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai,
Upelelezi wa makosa ya jinai, Usalama barabarani na stadi za kazi.
Taarifa za awali kutoka ndani ya chuo
hicho, zinaeleza kuwa mahafali hayo ya Polisi yatatanguliwa na medani
za kivita yatakayofanyika Julai 25 huko katika Kijiji cha Kilele-Pori,
Wilaya ya Siha.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment