MOTO wa tozo mpya ya kadi ya simu ya sh 1,000 kwa mwezi, unazidi kukielemea Chama cha Mapinduzi.
Wakati viongozi waandamizi wa CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
chama hicho, Nape Nnauye, akitoa msimamo wa kuitaka serikali kusitisha
uamuzi wa tozo hiyo, huku Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama
hicho, Mizengo Pinda, akiponda waziwazi kauli hiyo, mbunge wa Ubungo,
John Mnyika, ameibuka na kudai kuwa hiyo ni
ishara ya wazi kuwa serikali
inayumba.
Wiki hii Pinda alisema kuwa wanaopinga kodi hiyo hawana jema, kwa kuwa
tozo hiyo sio ya kuwaumiza wananchi bali mapato yake yatakwenda moja
kwa moja kusaidia kueneza umeme vijijini.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana Mnyika (CHADEMA), alisema
kutokana na kusigana kwa viongozi hao ni muhimu Rais Jakaya Kikwete kwa
nafasi yake anapaswa kuziba ombwe la uongozi lililopo na kutoa mwelekeo
kwa maslahi ya wananchi.
Alisema kuwa ni vizuri Pinda akajieleze au ajiuzulu kutokana na kauli yake na viongozi wenzake kutofautiana.
“Kauli hii ni tofauti na maelezo yake na ya wenzake katika mkutano
uliomalizika bungeni ambapo ilielezwa kwamba serikali inaanzisha tozo
mpya ya mafuta ya petrol (petroleum levy) ya sh 50 kwa lita na mapato
yake yatagharamia mahitaji ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA),” alisema.
Alisema kuwa wakati Waziri Mkuu Pinda akisema hayo, Waziri wa Fedha
na Uchumi, Dk. William Mgimwa, alisema kwamba serikali inaendelea
kupokea maoni kwa wadau na wananchi kwa ajili ya kurekebisha kodi hiyo.
Huku Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame
Mbarawa akikaririwa akizungumzia ushuru huo na kusema kuwa serikali
itahakikisha wananchi hawabebeshwi mzigo usiokuwa na sababu.
Mnyika alionyesha kutofautiana kwingine ni kwa Naibu Waziri wa Wizara
hiyo January Makamba ambaye alisema kwamba wizara yao ilipinga kodi hiyo
tangu awali na kupita kwake ilikuwa ni kutokana na kuzidiwa nguvu na
kwamba haliwezi kutekelezeka.
Alisema kuwa Baraza la mawaziri linaongozwa na misingi ya uwajibikaji
wa pamoja hivyo kwa utata wa kauli hizo zinazopingana, ni wazi hakuna
kauli moja ya serikali.
“Rais Kikwete anapaswa kushughulikia udhaifu huo kwa kutoa msimamo
wenye mwelekeo wa serikali kuwasilisha bungeni muswada kwa hati ya
haraka kufuta kodi hiyo na kupendekeza vyanzo mbadala vya kuziba pengo
kuhakikisha miradi ya maendeleo.”
Alisema Waziri Mkuu Pinda anapaswa kueleza iwapo wananchi wana sababu
ya kuendelea kuwa na imani naye katika mazingira haya ya serikali kutoa
maelezo tofauti bungeni na nje ya Bunge.
Alisema Pinda ndiye mwenye mamlaka na madaraka ya udhibiti, usimamiaji
na utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za serikali
anapaswa kueleza sababu za yeye na mawaziri wake kutofautiana hadharani
na ni kwa nini wasijiuzulu na baraza la mawaziri livunjwe.
Alisema kuwa kwa madaraka ya Rais ibara ya 33 ya Katiba ya nchi na
watumishi wote wa serikali kwa mujibu wa ibara ya 35 wanafanya kazi kwa
niaba yake anapaswa kutumia mamlaka yake, anayo haki ya kuwaondolea
mzigo huo mwingine usiokuwa wa lazima wa gharama za maisha wananchi.
“Ubovu wa Katiba ya nchi ibara ya 99 umetoa mwanya wa mamlaka makubwa
kuwa kwa Rais kuhusu kutoza kodi au kubadilisha kodi ambapo imeelekezwa
wazi kwamba Bunge haliwezi kushughulikia masuala hayo isipokuwa
kupunguza mpaka Rais awe amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe
na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na
waziri,” alisema.
“Rais Kikwete atoe msimamo wa kuwasilisha muswada kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi,” alisema.
Alisema kuwa Rais Kikwete afanye hivyo kwa kuwa serikali kupitia
mipango yake na ilani ya uchaguzi ya chama hicho iliahidi maisha bora
kwa kila Mtanzania kuanzia mwaka 2005 lakini tangu wakati huo kumekuwa
na maisha magumu kwa wananchi walio wengi.
Mnyika alisema kuwa kuwepo kwa udhaifu katika uzalishaji, usambazaji
wa bidhaa muhimu nchini, soko ‘holela’ na ongezeko la uagizaji wa
bidhaa kutoka nje, hali hii inachangiwa pia na ongezeko la kila mwaka la
kodi.
Alisema kuwa katika bidhaa na huduma zinazotumiwa na wananchi walio
wengi, serikali inapaswa kupanua wigo wa vyanzo mbadala vya mapato.
“Hali hii ilianza hata kabla ya kupitishwa kwa muswada wa Sheria ya
Fedha Juni 28, ya mwaka huu ambao ulisainiwa na Rais Kikwete kwa ajili
ya kuanza kutumika Julai 1, 2013,” alisema.
Alisema kuwa malalamiko ya muda mrefu ya wananchi ni namna
walivyosaini fomu za madai ya kutaka Bunge liingilie kati kuisimamia
serikali kudhibiti na kupunguza athari za ongezeko bei na gharama za
maisha.
“Kabla ya kuanza kwa mkutano wa 11 wa Bunge Aprili 8, 2013 nilikuwa
tayari nimepokea orodha ya watu waliosaini fomu zaidi ya 18,000 na
niliwasilisha taarifa ya ombi hilo la wananchi, hata hivyo halikuweza
kujibiwa kwa ajili ya kujadiliwa bungeni kwa kuwa mkutano huo ratiba
yake ilijikita katika Bajeti ya Serikali,” alisema.
Serikali ilipaswa kusoma alama za nyakati na kuitumia bajeti ya mwaka
2013/2014 na muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2013 kama zana ya
kutekeleza dhana ya kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kuweka
mkazo sio tu kwenye miradi ya maendeleo ya kuongeza uzalishaji.
Alisema kuwa badala ya kuchukua hatua hiyo serikali ikaendeleza
kuongeza kodi kwa sehemu kubwa kwa vyanzo vile vile na vingine vyenye
kuwalenga wananchi walio wengi.
“Katika hali hiyo ambayo ilinifanya kwenye mchango wangu bungeni Juni
27, 2013 niuite muswada wa sheria ya fedha kuwa ni ‘muswada wa majanga’
wenye kuongeza gharama za maisha ya wananchi kutokana na ongezeko kubwa
la kodi kwenye simu na mafuta,” alisema.
Alisema hayo alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Songea juzi, katika ziara yake ya wiki moja mkoani Ruvuma.
Pinda alisema, “Ni kama vile tozo iliyoongezwa kwenye mafuta ya
petroli, ambayo imetupa fedha nyingi katika mfuko wa barabara za
kuunganisha miji na mikoa.”
Aliongeza: “Nani asiyetaka vijiji vipate umeme kama miji, ili usaidie
kuondoa giza, uendeshe viwanda vidogo vidogo na usaidie kukuza uchumi?
Wanaopinga tozo hii, hawatutakii mema,” alisema Pinda.
TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment