Ikiwa
ni takribani mwezi mmoja tu tangu bomu lilipolipuka kwenye mkutano wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mkoani Arusha, jana tukio
kama hilo lilitokea jijini Dar es Salaam kwenye mkutano wa Mbunge wa
Ubungo (Chadema), John Mnyika, ambao aliutishia kwa lengo la kuwaelezea
wananchi mrejesho wa yaliyojiri bungeni hivi karibuni na kuhamasisha
wananchi kushiriki kutoa maoni kwenye rasimu ya Katiba mpya.Tofauti
na Arusha, jana bomu hilo lililipuka likiwa kwenye gari la Polisi
waliokuwa kwenye mkutano huo katika viwanja vya Sahara, katika Kata ya
Mabibo jijini Dar es Salaam na kuibua taharuki kubwa kwa wananchi na
wafuasi wa Chadema waliokuwa wamehudhuria mkutano huo.
Polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba bomu hilo lililipuka kwa bahati mbaya na kwamba ni la jeshi hilo.
Akizungumza
na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya
Kinondoni, Yusuf Mrefu, alisema mlipuko huo ulitokea kwa bahati mbaya na
kwamba haikuwa nia ya polisi kutumia nguvu au kuzuia mkutano wa
Chadema.
"Ni bomu
la mkononi. Polisi walikuwa na mazungumzo na viongozi wa Chadema na
siyo kwamba kulikuwa na vurugu au matumizi ya nguvu, ni tukio la bahati
mbaya," alisema.
Mrefu alisema pia kwamba Polisi haikuwa imepanga kupiga mabomu kwenye mkutano huo wala kuuzuia.
"Siwezi
kueleza limetengenezwa wapi, ni aina gani au kazi yake; kwa sababu mimi
mwenyewe nimepewa taarifa kwa simu, sikuwa eneo la tukio, nilikuwa
kwenye msafara wa Makamu wa Rais," alisema.
Aidha,
Kaimu Kamanda huyo bila kufafanua alisema: "Halina madhara." Hata hivyo,
alipoulizwa kazi ya bomu hilo ikiwa halina madhara, alijibu kwamba
asingeweza kueleza zaidi kwa kuwa hakuwa na taarifa za kina kwa kuwa
hakuwa eneo la tukio.
Hata alipoulizwa jina la kitaalamu la bomu hilo alisema hana taarifa za kina.
Wakati
Polisi wakieleza hayo, mashuhuda pamoja na taarifa zilizosambazwa kwenye
mitandao ya kijamii zilidai kwamba mtu mmoja alijeruhiwa kwenye tukio
hilo.
Taarifa
zinaeleza kwamba mlipuko huo ulitokea baada ya Mnyika kwenda kwenye gari
ya Polisi kwa nia ya kuwasalimia na ndipo kishindo kilichoashiria
mlipuko wa bomu kilisikika.
Kufuatia tukio hilo, mkutano huo ulipigwa marufuku na kuhamishiwa eneo la Ubungo Mataa ambako ulifanyika.
Diwani
wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob, akifungua mkutano huo alisema
waliamua kuchukua vibali viwili vya mkutano huo kwa tahadhari cha Mabibo
na cha Ubungo.
Akizungumzia
kuhusu tukio hilo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika
Ubungo jana, Mnyika alidai kuwa waliomba kibali cha kufanya mkutano huo
siku tano kabla kwa kuwaandikia polisi barua, lakini hawakuwajibu hadi
jana asubuhi wakiwataka kusitisha kwa sababu kulikuwa na ziara ya Makamu
wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, kukagua shughuli za usafi jijini
Dar es Salaam.
Mnyika
alisema aliwajibu polisi kuwa hawezi kupokea taarifa za kusitisha
mkutano wake huyo kwa simu bali aliwataka wampe kwa maandishi.
Alisema baadaye polisi waliandika barua ya kumuagiza asitishe mkutano wake huo kupisha ziara ya Makamu wa Rais.
Alisema
hata hivyo, alipoangalia ratiba ya ziara ya Makamu wa Rais, aligundua
kuwa haikugusa jimboni mwake na kuwaomba tena polisi wamruhusu kufanya
mkutano huo.
Alisema
alimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova
na kujibiwa yuko nje ya nchi, hivyo aliwaomba wasaidizi wake wampe
kibali lakini hawamkujibu na kumuomba asubiri wajadiliane kwanza.
Mnyika
alisema kutokana na muda kuyoyoma, alimtafuta Mkuu wa Jesh la Polisi
nchini, Inspekta Jenerali Said Mwema, kumuomba amsaidie, lakini aligonga
mwamba baada ya kumjibu kuwa hawezi kutengua maamuzi yaliyotolewa na
kiongozi wake wa chini na kumtaka aandike barua nyingine ya kuomba
kibali cha kufanya mkutano.
"Wakati
naendelea kuwasiliana na viongozi wa polisi kuomba wanipe kibali,
nilikuwa tayari kwenye viwanja vya Sahara na ndipo zikaja defender
(magari ya polisi) tatu za polisi," alisema na kuongeza kuwa:
"Ziliposimama
niliwafuata na kwenda kuwaambia kuwa vipi tena mbona mmekuja wakati
nimeomba kibali cha kufanya mkutano, ndipo lilipolipuka bomu hilo ndani
ya gari ambalo nami nilikuwa nimesimama karibu nalo."
Alisema
baada ya kulipuka bomu hilo, watu walikuwa wamekusanyika katika viwanja
hivyo walikumbwa na taharuki na kukimbia ovyo kunusuru ya maisha yao.
Kwa mujibu wa Mnyika, wakati watu hao wakikimbia ovyo, alikwenda
lilikoangukia bomu hilo kumuwahi majeruhi, Thomas Jarome.
Alisema
polisi nao walikwenda kumuwahi majeruhi huyo na kumbeba 'mzobemzobe'
wakati wakitaka kumuingiza kwenda gari lao, Mnyika na viongozi wengine
wa Chadema waliwazuia na kumpeleka hospitalini ambako alipatiwa matibabu
na kuruhusiwa kuondoka.
Alisema
wakati majeruhi huyo akiendelea kupatiwa matibabu, viongozi wa chama
hicho walikusanyika na kujadili sehemu nyingine ya kwenda kufanyia
mkutano wao na kubaini kuwa Diwani wao wa Ubungo alikuwa na kibali cha
kufanya mkutano eneo la Abiani Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Aliwatangazia wananchi wafuasi na wapenzi wa Chadema wakiwaomba wahamie Abiani.
Katibu wa
Mbunge wa Ubungo, Gastone Garubindi, alidai bomu hilo lilipigwa na
polisi kwa lengo la kuwatisha wananchi wasihudhurie mkutano huo.
Akizungumza
na NIPASHE majeruhi Jerome, alidai kuwa polisi walikusudia kulipua bomu
hilo kwani lilikuwa mikononi mwao na askari waliopata mafunzo ya
kutosha kuhusu milipuko.
Alisema
baada ya kujeruhiwa, viongozi wa Chadema walimpeleka katika kituo Mabibo
ambako alipewa PF3 na kwenda zahanati Tandale na kutibiwa.
Jerome
alisema baada ya kutibiwa aliruhusiwa kurejea nyumbani na kutakiwa
kurudi leo kwa uchunguzi zaidi na kuchomwa sindano ya pepopunda
(tetanus).
Tukio la
jana limekuja huku uchunguzi wa mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15, mwaka
huu katika viwanja vya Soweto, Kata ya Kaloleni mkoani Arusha kwenye
mkutano wa kufunga kampeni za udiwani wa Chadema, ukiwa bado unaendelea.
Katika tukio hilo, watu watatu walipoteza maisha na wengine kadhaa
kujeruhiwa vibaya. Bomu hilo linaelezwa kuwa lilipuka kwenye mkusanyiko
wa watu mita chache kutoka jukwa kuu, wakati mkutano huo ulipokuwa
umekwisha na shughuli ya kukusanya michango ikiendelea.
Viongozi wa juu wa Chadema, Freeman Mbowe na Godbless Lema walikuwapo kwenye eneo hilo.
Hadi sasa
hakuna mtu ambaye amekamatwa kuhusiana na mlipuko huo pamoja na kwamba
Serikali imetangaza donge nono la Sh. milioni 100 kwa mtu
atakayefanikisha kukamatwa kwa mhusika au wahusika wa tukio hilo.
Zaidi ya watu 70 walijeruhiwa baada ya tukio hilo kufuatia polisi
kufyatua risasi za moto kwa nia ya kukabiliana na wananchi waliokuwa
wanawashambulia.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikaririwa akieleza kwamba bomu lililolipuka Arusha lilitengenezwa China.
Aidha,
Septemba, 2012 aliyekuwa Mwakilishi wa Kituo cha Chanel Ten mkoani
Iringa, Daudi Mwangosi, aliuawa kwa kupigwa bomu la machozi na askari wa
Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) eneo la Nyololo Wilaya ya Mufindi
mkoani Iringa.
Alipigwa
bomu hilo baada ya kupokea kipigo kutoka kwa baadhi ya askari wa FFU
waliokuwa wakiizuia Chadema kuendesha harakati zake za kufungua tawi la
chama hicho katika eneo hilo.
Mwangosi
ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa
Iringa (IPC), aliuawa mbele ya wananchi, askari wa FFU na aliyekuwa
Kamanda wa jeshi hilo mkoani humo, Michael Kamuhanda.
Askari
huyo anayedaiwa kumuua Mwangosi, Pacificus Cleophase Simon (23),
alikamatwa na kufikishwa mahakamani akikabiliwa na tuhuma za mauaji hayo
na kesi hiyo bado inaendelea kutajwa.
0 comments:
Post a Comment