na. Neema Kishebuka:
UKIFIKA katika kijiji cha Pori na kutaja jina la Dk. Japhet
Kirilo linafahamika kwa watu wa rika zote wa kabila la Wameru kutokana na
historia yake enzi za uhai wake katika kutetea maslahi ya watu wa Meru.
Baada ya kufika katika kijiji hicho nikiwa na baadhi ya
viongozi kadhaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tunakutana na
Nderetwa Kirilo ambaye ni mke wa Dk. Kirilo na anatukaribisha nyumbani kwake na
kuanza kutupa ramani fupi huku akiwa na tabasamu.
“Hapo unapopaona ndipo mahala ambapo alikuwa anakaa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akimtembelea mume wangu wakati wa kudai
uhuru toka kwa wakoloni,’’ anaanza kueleza Nderetwa (85) wakati alipotembelewa
na wabunge Vicent Nyerere (Musoma Mjini), Mchungaji Islael Natse (Karatu) na
viongozi wengine wa CHADEMA wakiongozana na mgombea ubunge wa Arumeru Mashariki
kupitia CHADEMA, Joshua Nassari.
Anaanza kueleza historia fupi ya Mzee Kirilo huku akimshika
mkono Vicent na kusema, “Baba yako alikuwa mcheshi sana alipenda kunitembelea
kila wakati alipokuwa anafika Meru.
Alikuwa anapenda nyama ya kuchoma, alikaa katika chumba
hicho na kulala siku zote alipokuwa hapa,” huku akionyesha chumba ambacho kwa
sasa amekifanya sebule huku mlangoni kukiwa na picha ya Mwalimu Nyerere.
Anasema Dk. Kirilo alikuwa daktari wa magonjwa ya binadamu
na alikuwa rafiki kipenzi wa Mwalimu Nyerere, lakini kutokana na mapenzi yake
makuu kwa watu wa kabila la Meru, aliamua kuacha kazi ya kuajiriwa na kupigania
haki ya Wameru kwa kudai ardhi iliyokuwa ikishikiliwa na wakoloni.
“Dk. Kirilo alichangiwa pesa na Wameru kwenda kudai ardhi
Umoja wa Mataifa, lakini hakufanikiwa kwa kuwa ilionekana Meru haikuwa katika
orodha ya mataifa koloni, kwa kuwa haikuwa nchi, akaamua kurudi kuungana na
Mwalimu Nyerere kuhakikisha wanawaondoa wakoloni.
“Mwalimu Nyerere alikuwa anafika nyumbani hapa mara kwa mara
kuja kupanga mipango ya ukombozi na alikuwa analala hapahapa na nilikuwa
nawapikia chakula kabla hawajaelekea katika shughuli zao za ukombozi. Nashukuru
Mungu walifanikiwa baada ya miaka kama nane tulipata uhuru, hata alipofariki
mume wangu, Mwalimu alihuzunuka mno na alikuja msibani,” anasema.
Anasema kabla ya safari hiyo ya Umoja wa Mataifa, mbele ya
nyumba yao waliweka chungu ambapo kila mtu alichangia kiasi chochote cha fedha
na zilipopatikana za kutosha alituma kama nauli kwenda Umoja wa Mataifa kudai
ardhi ya kabila lake mwaka 1952.
Bibi huyo ambaye ana watoto 10 aliozaa na Dk. Kirilo,
anasema mumewe alizaliwa mwaka 1921 na kufariki Mei 30, 1997.
Anasema jina Kirilo ni kubwa katika kabila la Wameru na
kutokana na heshima yake, ataendelea kukumbukwa na kuenziwa kwani alipenda
kuona kabila hilo halionewi wala kunyanyaswa.
Hata hivyo, anaeleza masikitiko yake kuwa Meru iliyokuwa
ikipiganiwa na Kiliro sasa inataka kupoteza maadili yake na kuongeza kuwa hata
Mwalimu Nyerere na Kirilo wangeamka leo hii wangeshangaa jinsi ardhi ya Meru
ilivyoingiliwa na wageni ambao wamehodhi maeneo makubwa.
“Laiti leo hii Mwalimu Nyerere angeamka na kukuta ardhi yetu
walivyopewa wawekezaji kulima maua badala ya mazao sijui ingekuwaje,’’ anasema.
Anasema mfano mzuri ni mashamba yaliyochukuliwa kwa ajili ya
kupandwa maua huku Wameru wenyewe wakikosa maeneo ya kulima mazao.
“Wazee waliipigania mno ardhi ya Meru na ndiyo maana
waliweza kwenda mbali zaidi kuhakikisha wakoloni wanaachia ardhi yetu, lakini
vyote hivyo vimesahaulika kwa sasa,’’ anaeleza kwa masikitiko.
Mbele ya nyumba ya mpigania uhuru huyu ambaye bado ameacha
historia kubwa katika kabila hili ndipo lilipo kaburi lake ambapo eneo hilo
limezungushiwa uzio na kujengewa ngao kubwa.
Wageni mbalimbali wamekuwa wakifika nyumbani hapo kuzulu
kaburi la shujaa huyo aliyekuwa na uchungu wa kuona kabila lake linabaki kuwa huru,
ndoto ambayo ilikuwa kweli mwaka 1961.
Leo hii mashujaa hao hawapo imebaki historia ambayo
itaendelea kuendelezwa siku hadi siku kwa vizazi vijavyo na uwepo wa kaburi
hilo katika kata ya Pori ni moja ya kumbukumbu itakayokumbukwa daima na watu wa
kabila la Meru na taifa kwa ujumla.
wonderful
ReplyDeleteTutakukumbuka mno mtetezi wa Meru,R.i.p Mzee Krilo.Miss you father.
ReplyDeleteStory mzuri sana ila rekebisha hapo mwanzo ni Poli sio Pori
ReplyDeleteKazi mzuri sana
Historia ya Mzee Kirilo ni yakishujaa sana iliyojaa uzalendo