TASNIA ya
muziki wa kizazi kipya Bongo kwa sasa imeshika kasi, wasanii kwa kiasi kikubwa
wameweza kuwekeza na hata majina yao yamekuwa juu kiasi cha kujijengea imani
kubwa mbele ya jamii.
Imani hii kubwa na ushabiki uliokithiri,
imezua jambo jingine kubwa ambalo limekuwa tatizo la kimaendeleo. Tatizo hilo ni
wasanii kujikuta wakiendeshwa na umaarufu wa majina yao katika namna ya
wanavyoishi.
Imebainika kwa kuwa majina yao ni makubwa
kuliko uwezo wao wa kuishi. Jambo hili limewafanya wasanii hao waishi maisha
feki mbele ya jamii yao.
Kwa kuishi maisha hayo, wamejikuta
wakitumia gharama kubwa katika kuishi maisha ambayo si ya daraja
lao.
Mavazi
Ukianzia na mavazi, kwa kuwa tu anajulikana
yeye ni yule msanii aliyeimba wimbo fulani maarufu, basi hata kama hana mavazi
ya gharama atajitahidi hata kwenda kuazima, ili mradi mashabiki wake wakimwona
wamkute nadhifu.
Awali tabia hiyo ilidhaniwa ni ya wasanii
wa dansi pekee hasa Wakongomani, lakini sasa ni fasheni kwenye
Bongofleva.
Inakubalika na ni dhahiri unadhifu kwa watu
wenye mvuto kwa jamii ni jambo lililo wazi, lakini unadhifu unahusiana vipi na
gharama?
Wengi wanapotelea hapa, wanafikiri unadhifu
ni kuvaa vitu vyenye gharama kumbe uchaguzi wa vitu vya kawaida na mpangilio
vinaweza kukufanya kuwa nadhifu kuliko vitu ghali.
Angalia mavazi ya Michael Jackson, yalikuwa
ya gharama sana lakini si kweli kwamba mavazi yale ndiyo yalikuwa yakisababisha
aonekane nadhifu kuliko wasanii wote duniani, alikuwa tu ni Mfalme wa
Pop.
Lakini Bongo ukiachilia mbali kuazimana,
kuvaliana na kuambukizana magonjwa, kuna kundi kubwa la wasanii ambao hupenda
kujihusisha na maduka ya nguo ili mradi tu wapate kupendeza.
Usafiri
Ukishakuwa staa, tayari kuitwaitwa
barabarani, kufuatwa na watoto ukiwa katika matembezi yako, ama kuombwa kupiga
picha na mashabiki wako na mambo mengineyo kama hayo ni jambo la
kawaida.
Wasanii wetu wanahisi hii ni ghasia na
kuwakimbia mashabiki wao. Huukimbia kabisa usafiri wa umma, yaani daladala au
wakati wanaenda mikoani huona bora hata wakodi magari badala ya kupanda
basi.
Kuna asilimia kubwa ya wasanii tunaowaona
wanaendesha magari kana kwamba wanayamiliki, kumbe si yao. Wengi huyakodi ili
wakionana na mashabiki wao angalau waonekane wao ni wa matawi ya
juu.
Jina linaendelea kuwa kubwa huku mhusika
akiteseka kwa kuingia madeni makubwa.
Amini usiamini humu ndimo asilimia kubwa ya
kipato cha msanii wa kizazi kipya kinapopotea. Magari hukodishwa kuanzia Dola 25
mpaka Dola 40 kwa siku kulingana na aina ya gari.
Makazi
Hapa ndipo ambapo hawajali kabisa, wengi
wao huishi kwa kutegemea wazazi na wengine huishi kwenye nyumba za kupanga kwa
kuchangia au kukaa tu kwa mtu huku wakiamini ipo siku mambo yatakuwa sawa
wajenge.
Nyumba wanazoishi wengi wao ukiangalia na
mavazi wanayovaa na magari wanayoendesha ni vitu tofauti. Wengi huweka
kipaumbele mwonekano wa nje kuliko hata wanapoweka ubavu.
Ni wasanii wachache wanaomudu maisha yao
kutokana na kipato kilivyo.
Ukiangalia mavazi, usafiri na huku anataka
kuonekana kila sehemu ya starehe, sehemu ya pato hupotea huko na mwisho wa siku
hubakia kuwa na umaarufu wa maneno na sifa za mdomoni .
Biashara?
Wengi zimewashinda kutokana na ukweli
kwamba hawana uzoefu na tija katika biashara. Huanzisha miradi kwa kasi kwa
kushirikiana na watu, lakini huwa hawachukui muda kwani hujikuta wakitolewa nje
kutokana na matumizi yao makubwa kuliko kipato.
Sifa kubwa ya mfanyabiashara ambaye
anasimama kama mchumi ni kuzijua hesabu zake kwa umakini jambo ambalo wasanii
wetu wa kizazi kipya hawana.
Ukiachana na hilo, wengi wamekuwa
wakitumiwa tu majina yao katika maduka lakini ukija kwenye ukweli, maduka huwa
si yao, majina hayo hutumika kunufaisha biashara za watu na mwisho wa siku
ukweli huja kubainika.
Upo mfano wa msanii mmoja aliyewahi kuwa na
Baa maeneo ya Sinza, lakini ukweli ukaja kugundulika kwamba baa ilikuwa ni ya
mwanamke aliyekuwa na uhusiano naye, pale walipoachana ndiyo siri
ikavuja.
0 comments:
Post a Comment