Siku moja
baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuagiza matangazo ya
Star TV yarejeshwe kwenye kisimbuzi cha Star Times ifikapo saa 10 jioni
jana, televisheni hiyo imegomea agizo hilo na imetishia kwenda
mahakamani ikiwa italazimishwa kurejea humo.
Taarifa ya kugoma agizo hilo, ilitolewa jana na Meneja Mipango na
Utafiti wa Sahara Media Group Ltd, Kampuni inayomiliki Star TV, Nathan
Lwehabura.
Ilieleza kuwa kinachofanywa na TCRA, kuwalazimisha kurejesha
matangazo Star Times ni ukiukwaji wa Sheria ya Hatimiliki na Sheria ya
Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010.
"Serikali ya Tanzania ni mwanachama wa WTO na pia WIPO (World
Intellectual Property Rights Organization) na hivyo kwa kulazimisha
uvunjaji wa sheria za hati miliki ina maana inavunja haki zetu zilizopo
kikatiba! Tutakwenda mahakamani kupata haki yetu hii muhimu," ilieleza
sehemu ya taarifa hiyo.
Pamoja na kutoweka bayana lini watakwenda mahakamani, Lwehabura
alisema sheria ya hati miliki inaweka kinga kwa vipindi vya redio,
televisheni, nyimbo na sanaa. Alisema kulazimisha Star Times kupora
vipindi vya Star TV, inadhihirisha kilio cha wasanii wa Tanzania,
wasivyolindwa na Serikali yake.
Taarifa hiyo
ilieleza Mei 23 mwaka huu, Star TV kupitia mwanasheria wake iliwataka
Star Times kuiondoa kwenye kisumbuzi chao ifikapo saa sita usiku wa Mei
31, mwaka huu kutokana na kurusha na kuuza maudhui na vipindi vyake bila
idhini na kukiuka sheria za haki miliki (Copyright laws).
"Katika barua hiyo, Star TV iliwakumbusha Star Times kwamba hawakuwa
na mkataba wa kurusha kituo hicho kwa mujibu wa sheria ya EPOCA, pia
hawana haki ya kutumia maudhui yake bila idhini chini ya Sheria ya Haki
miliki ya Tanzania na kimataifa," ilieleza taarifa hiyo.
Hata hivyo, Mei 31 Star Times/Star Media walijibu kwamba hawajakiuka
sheria yoyote. Walisisitiza wataendelea kuirusha Star TV, kutekeleza
matakwa ya sheria ya EPOCA na kanuni zake. Lakini, Star TV iliwaandikia
tena na kuwaeleza itachukua hatua zaidi kwa kukiuka ;na kuwataka
iwaondoe saa sita usiku wa Juni 8, mwaka huu.
Tarehe 6 Juni mwaka huu, Star TV iliwaandikia tena Star Times
ikisisitiza nia yake ya kuchukua hatua zaidi, kutokana na wao kuendelea
kukaidi ombi hilo na kuainisha mapungufu kadhaa ya kisheria kwa upande
wao, yanayoifanya Star TV ijiondoe kwenye king'amuzi chao ifikapo saa
sita usiku wa tarehe 8 Juni, mwaka huu na kufanya hivyo.
Jana, TCRA, kupitia Mkurugenzi Mkuu, Profesa John Nkoma, iliagiza
chaneli hiyo irejeshwe mara moja jana ifikapo saa 10 jioni na kuzitaka
pande hizo mbili, kukutana na mamlaka Juni 17 mwaka huu kwa majadiliano
zaidi.
Hata hivyo, mpaka jana saa 11.20 jioni, Star TV haikuwa inaonekana
kwenye Star Times huku TCRA ikidai Star TV inakiuka sheria ya EPOCA na
ikikaidi, itachukuliwa hatua kwa kuwa si yenyewe wala Star Times walioko
sawa katika maamuzi hayo.
TCRA iliwataka watoa huduma hao kufuata Sheria, inapotokea
kutokuafikiana katika jambo fulani badala ya kutoa maamuzi bila
kumshirikisha Mdhibiti (TCRA), kwani kufanya hivyo ni kuwakosea haki
wananchi.
Hata hivyo, Star TV imesema haipo tayari kuona maudhui yake yakiuzwa
nje ya nchi bila makubaliano. Star Times jana hawakuwa tayari
kuzungumzia suala hilo. Lakini, awali, Msaidizi wa Meneja wa Star Times,
Hellen Elisa alithibitisha kujitoa kwa Star TV. Alisema waliwaandikia
barua na kudai wamejitoa kwa matakwa yao.
SOURCE> http://audifacejackson.blogspot.com/2013/06/star-tv-wagoma-kurudisha-matangazo-yao.html
SOURCE> http://audifacejackson.blogspot.com/2013/06/star-tv-wagoma-kurudisha-matangazo-yao.html
0 comments:
Post a Comment