HUKU Albert Kenneth Mangwea ‘Ngwea’
akiwa kaburini siku ya pili leo kufuatia kufariki dunia ghafla
usingizini nchini Afrika Kusini, Mei 28, mwaka huu, mambo matano ya
kushangaza yamezuka katika kipindi chote cha msiba, Risasi Jumamosi
linakupa kila kitu.
Kwa mujibu wa utafiti wetu wa kina, waombolezaji mbalimbali wamekuwa
wakiyazungumzia mambo hayo huku wengine wakihoji kuwepo kwake.
1. RIPOTI YAFICHWA KIBINDONI
Usiku wa kuamkia mazishi yaliyofanyika kwenye Makaburi ya Kihonda,
Morogoro, paparazi wetu alipata bahati ya kuzungumza na mama wa marehemu
Ngwea, Denisia Mangweha.
Katika mazungumzo hayo, mwanahabari wetu alimuuliza mama huyo kama
alikuwa amekabidhiwa ripoti ya daktari inayotatua fumbo la nini kilimuua
Ngwea.
Haya hapa majibu ya mama huyo:
“Sijapata wala sijui chochote kuhusu hiyo ripoti, wala sijui nani anayo.”
Jumanne iliyopita, ilidaiwa kuwa Mtangazaji wa Clouds FM, Millard Ayo
aliyekuwa ‘Sauzi’ ndiye aliyekabidhiwa ripoti hiyo ambapo na yeye
aliikabidhi kwa ndugu wa marehemu.
Kwa kawaida, ripoti inayoweka wazi kiini cha kifo cha marehemu
husomwa siku ya mazishi, jambo ambalo halikufanyika siku ya kumzika
Ngwea.
MANENO YA WATU MAKABURINI
Baadhi ya waombolezaji waliokuwa makaburini hapo, walitoa hisia zao
wakidai kwamba, inawezekana ripoti hiyo haikuwa nzuri hivyo ili kulinda
heshima ya marehemu ililazimika kuiacha kibindoni.
2. MAMA WA MAREHEMU AMTAMBUA DEMU MZUNGU
Jumatano, siku moja kabla ya mazishi, mama wa marehemu alimshika
mkono aliyekuwa mchumba wa marehemu, yule mwanamke Mzungu akisema Albert
(Ngwea) alikuwa akienda naye nyumbani hapo (Morogoro).
Alisema mara kadhaa walitoka yeye, marehemu na Mzungu huyo kwenda
kula ‘bata’ mahali kabla ya kurejea Dar. Kwa hiyo Mzungu ni mwanamke
aliyekuwa akitambulika na mama wa marehemu.
Cha kushangaza, dada wa marehemu aitwaye Neema Mangweha, alisema
mchumba wa marehemu anayemjua yeye anaitwa Siwema ambaye kwa sasa ana
ujauzito wa mwanamuziki maarufu wa muziki wa kizazi kipya Bongo.
3. MTOTO WA MAREHEMU AIBUKIA MAKABURINI
Alhamisi, wakati msafara wenye mwili wa marehemu ukiwa makaburini,
mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Paulina Jeremiah akiwa na
mtoto wa kike alijitokeza hadharani na kukutana uso kwa uso na paparazi
wetu akidai mtoto huyo ni wa marehemu Ngwea.
Mwanamke huyo, mkazi wa Kigamboni, Dodoma alisema mtoto huyo anaitwa
Neema Albert, alimzaa mwaka 2001 wakati huo Ngwea alikuwa akisoma
Sekondari ya Mazengo.
Wakati anajieleza hayo, ndugu wawili wa marehemu walitokea, mmoja akiitwa Anthony Kenneth Mangweha na kumsikiliza mama Neema.
Anthony alimuuliza mama Neema kama kuna ndugu yeyote wa marehemu anayetambua uwepo wa mtoto huyo, mama Neema akawataja.
Aliwataja vijana watatu kwa jina mojamoja, Frank, Jotam na Amani
ambapo alisema waliwahi kutumwa na marehemu kwenda Dodoma kumwangalia
mtoto huyo.
Anthony alikiri kuwa vijana hao watatu ni ndugu wa familia hiyo na
akamtaka mama Neema kupoa, baada ya mazishi na kurudi nyumbani watakaa
kuzungumzia suala hilo.
4. M 2 THE P AIBUKIA KWENYE KUAGA MWILI
Katika hali iliyowashangaza wengi, msanii wa Bongo Fleva aliyepata
matatizo na marehemu lakini yeye akapona, Mgaza Pembe ‘M 2 THE P’
aliibuka kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambako mwili wa
marehemu ulikuwa ukiagwa.
Baadhi ya watu waliomtambua msanii huyo walionekana kumshangaa sana huku wakihoji ametua lini kutoka Sauzi.
M 2 The P alishindwa kuhimili wakati anapita kwenye mwili wa
marehemu, alimwaga machozi, hali iliyosababisha waombolezaji wawili
kumshika kulia na kushoto na kumtoa eneo hilo.
MAVAZI YAKE SASA!
Kikubwa kilichoibua maswali kutoka kwa waombolezaji ni jinsi msanii
huyo alivyovaa. Wengine waliamini vaa yake ilisababishwa na kutaka
kujificha watu wasimtambue. Pia wapo waliodai inawezekana alitoroka huko
Sauzi.
Alivaa suruali ya ‘jinzi’, fulana ya mikono mifupi, miwani na kofia kubwa licha ya
hali ya hewa Morogoro kuwa si ya baridi sana kiasi cha kuvaa hivyo.
5. KUMBE MAREHEMU ALITUMIWA FEDHA SAUZI
Tofauti na mashabiki wake walivyoamini kuwa marehemu alikuwa akipiga
fedha ndefu Sauzi na kuzituma Bongo kwa wanafamilia, mmoja wa ndugu zake
alibumburua siri kuwa kuna wakati hali ilikuwa mbaya hadi ikabidi
amtumie shilingi laki moja na nusu.
“Watu wanadhani labda Albert (Ngwea) alikuwa mambo safi muda wote
Afrika Kusini kama vijana wengi wanavyoamini. Si kweli kuna wakati
kabisa alikuwa akinipigia na kuniambia hali ilivyokuwa mbaya,” alisema
ndugu huyo kwa sharti la kutotajwa gazetini.
0 comments:
Post a Comment