Blogger Widgets

Thursday, October 18, 2012

VURUGU ZANZIBAR ZA CHUKUA SURA NYINGINE, ASKARI AUAWA KINYAMA KUFUATIA VURUGU ZA WAFUASI WA UAMSHO.


 Kamishna wa Polisi Mussa Ali Mussa akifafanua jambo katika Mkutano na Waandishi wa Habari akielezea juu ya Fujo na Ghasia zilizotokea katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kupelekea kifo cha Askari Mmoja,Mkutano huo umefanyika hapo katika Makao Makuu ya Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.

 Mwandishi wa Habari wa Hits FM Mustafa akiuliza maswali katika Mkutano wa Jeshi la Polisi juu ya fujo na ghasia zilizotokea katika Mkoa wa Mjini Magharibi,hapo katika Makao Makuu ya Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa katika Mkutano wa Jeshi la Polisi kuelezea juu ya Fujo na Ghasia zilizotokea katika Mkoa wa Mjini Magharibi na kupelekea kifo cha Askari Mmoja,Mkutano huo umefanyika hapo katika Makao Makuu ya Polisi Ziwani Mjini Zanzibar.

 
Askari mmoja wa Jeshi la Polisi F.2105 Coplo Said Abdulrahaman wa Kikosi cha FFU Mkoa Mjini Magharibi ameuliwa kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi wakati akirudi kazini majira ya saa 6.30 usiku wa kuamkia leo katika eneo la Bububu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani leo, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa amesema mauaji hayo  yamesababishwa na fujo za wafuasi wa Jumuiya ya UAMSHO baada ya kuenea uvumi wa kutekwa Msemaji Mkuu wa Jumuiya hiyo Sheikh Farid Hadi usiku wa kuamkia jana. 
Kamishna Mussa amesema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kuwatafuta watu waliofanya mauaji ya Coplo Saidi Abdulrahaman ili kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani kama  sheria za nchi zinavyowaelekeza.
Amesema mpaka hivi sasa watu 10 wamekamatwa kwa tuhuma za makosa mbali mbali yaliyotokana na vurugu za jana na upelelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi wa kutekwa Sheikh Farid unaendelea. 
Ameongeza kuwa  kutekwa kwa Sheikh Farid kunatia mashaka kutokana na mazingira ya kutoweka kwake kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mdogo wake Said Omar Said ambae alikuwa dereva wake katika hatua za mwisho  maeneo ya Mazizini walipokwenda kununua umeme.
“Sheikh Farid alimuamuru Said amuache katika eneo hilo aende nyumbani kupeleka umeme na wakati huo akaendelea na mazungumzo na watu wengine  walikuwemo ndani ya gari nyengine ndogo ya NOAH  ambayo nambari zake hazijajulikana lakini aliporudi kumchukua hakumkuta” alisema Kamishana Mussa.     
Amesema fujo hizo zilisababisha hasara  kubwa kwa Serikali, Chama tawala na  wananchi ikiwemo kuchoma na kuharibumiundo mbinu ya barabara, kuharibu maskani za CCM za Kisonge na Muembeladu kwa kuzichoma moto baadhi ya magari kuvunjwa vioo na kuvunja duka la pombe na kuiba mali iliyokuwemo ndani. 
Hata hivyo amedai hali ya Mji wa Zanzibar kwa sasa ni shwari, wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vyengine vya ulinzi na usalama vitaendelea kuhakikisha amani inadumu muda wote.
Amewataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu na kudumisha amani na utulivu katika maeneo yao, na kutoa taarifa za watu waliohusika na  vurugu pamoja na  mauaji ya Coplo Said Abdulrahaman.      

0 comments:

Post a Comment