Blogger Widgets

Thursday, August 23, 2012

Hukumu Igunga Yaivuruga CCM



WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikitangaza kusudio lake la kukata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, iliyotengua ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Dk. Dalali Kafumu, wadau mbalimbali wameipongeza hukumu hiyo wakiita ni darasa tosha kwa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.

Miongoni mwa waliosifu hukumu hiyo ni pamoja na Spika mstaafu, ambaye pia ni Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akisema kuwa maamuzi hayo inafaa yaheshimiwe.

Akizungumza jana mjini Tabora, Sitta alisema kuwa mahakama ina mamlaka yake kisheria, hivyo wana CCM hawana budi kuyaheshimu maamuzi hayo kwani imefanya kazi yake inavyotakiwa.

“Kama kuna mtu anaona hukumu hiyo haikutenda haki, anaweza kwenda mahakamani kukata rufaa, lakini mimi nashauri ni vema tujipange upya tuingie ulingoni.

“Hapa mimi sina maoni juu ya jambo hilo, bali cha msingi ni vema tukakaa na kutafakari yaliyotokea huko Igunga, ili basi tukiona inafaa kukata rufaa sawa, na kama tuingie ulingoni, yote ni sawa,” alisisitiza Sitta.

Katika hukumu yake juzi, Jaji Mary Nsimbo Shangali, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa CHADEMA, Joseph Kashindye, alisema kuwa alipokea malalamiko 15 ambayo yaliridhiwa na pande zote mbili, lakini yakaongezwa madai mengine mawili na kufikia 17.

Mbali na Dk. Kafumu, washitakiwa wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Msimamizi wa uchaguzi jimboni humo, Protace Magayane na kwamba mahakama hiyo ilithibitisha madai saba ya kutengua matokeo hayo.

Hata hivyo, wakati Sitta akiwa na mtazamo huo, CCM kupitia kwa Katibu wake wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ilieleza kutoridhishwa na hukumu hiyo, hivyo kuamua kukata rufaa.

Pamoja na CCM kuchukua hatua hiyo, wadau mbalimbali wa masuala ya kisiasa na wanaharakati waliliambia Tanzania Daima kuwa, hukumu hiyo ni darasa tosha la demokrasia linaloonesha jinsi sheria za uchaguzi zinavyovunjwa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashir Ali, alisema hukumu hizo za uchaguzi ikiwamo hiyo ya Igunga, zina maana sana kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Msajili wa Vyama vya Siasa, wanasiasa na wananchi.

“Tatizo letu huwa hatusomi hukumu hizi kwa undani, kwani tungekwishajua kuwa ni darasa tosha la demokrasia. Suala la takrima lilikuwa halieleweki kama ni rushwa, ushindani wetu wa kisiasa si wa kuvumiliana, una matumizi makubwa ya fedha, mali za serikali na madaraka kwenye kampeni,” alisema.

Ali alifafanua kuwa hukumu hiyo imetoa mwanga kuwa, kama hakuna chombo huru cha kusimamia sheria zinazokiukwa ni sawa na bure, akitolea mfano Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa licha ya kuwapo wakati wa mchakato huo, vilishindwa kuchukua hatua.

“Kuna mjadala kuhusu uwepo wa sheria ya Tume ya Uchaguzi, maana tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi hakuna sheria ya Tume ya Uchaguzi, badala yake chombo hiki kinatambuliwa na sheria za uchaguzi, jambo linalotoa mwanya kwa mapungufu yanayojitokeza sasa,” alisema.

Kuhusu uwajibikaji wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wakati wa uchaguzi huo mdogo, Ali alisema kuwa mpaka sasa umuhimu wa ofisi hiyo hauonekani maana kama hoja ni kusajili vyama, kazi hiyo inaweza kufanywa hata mahakamani.

Alibainisha kuwa, kwa sasa ofisi ya msajili na Tume ya Uchaguzi ni kama idara tu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hivyo wananchi wanapaswa kutumia hukumu ya Igunga kama tathmini wakati huu wa mchakato wa katiba mpya kusahihisha makosa ya kuvifanya vyombo hivyo huru.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) Bara, Mtatiro Julius, alisema hukumu hiyo itawafungua wananchi kuona umuhimu wa kubadilisha mfumo wa uchaguzi ili kuepusha taifa kuingia gharama zisizokuwa za lazima pale kiongozi anapokufa ama kuenguliwa.

“Hii naiona kama hatufikirii sawa sawa, maana matumizi ya mabilioni ya fedha kwenye uchaguzi yalikuwa kwa vyama vyote kule Igunga hasa CCM, CHADEMA na CUF. Lakini hili linaweza kuepukwa mana kama upuuzi unafanywa na watu wawili, hatuna sababu ya kulisababishia taifa hasara,” alisema.

Kwa mujibu wa Mtatiro, inapotokea hali kama hiyo ya mbunge kuenguliwa au kupoteza maisha, mshindi wa pili kutoka chama kingine ndiye achukue nafasi badala ya kurudia uchaguzi.

“Igunga tuliona Dk. Kafumu walipishana kidogo na Kashindye wa CHADEMA, hivyo kwa vile huyu alikiuka taratibu, basi mshindi wa pili apewe nafasi kuliko kurudia uchaguzi, kwani kufanya hivyo kunaweza kukipa chama kilichoenguliwa ushindi tena wa mtu asiyefaa,” alisema Mtatiro.

Mwanasiasa huyo pia hakusita kuinyoshea kidole Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, akisema kuwa, John Tendwa (msajili) ameonesha wazi ni wakala wa CCM anayefanya mbinu za kukisaidia chama hicho kishinde badala ya kusimamia kanuni na sheria.

Mtatiro aliweka bayana kuwa makosa yaliyoainishwa kwenye hukumu iliyomtia hatiani Dk. Kafumu na kumnyang’anya ubunge wake, yalilalamikiwa mapema na wapinzani kwa Msajili wa Vyama wakati wa kampeni, lakini hakuchukua hatua yoyote.

“Msajili wa vyama hana meno, na huyu amekuwa na kashfa ya kusajili hata vyama visivyo na sifa ilimradi tu aweze kuvidhoofisha vyama makini vya upinzani. Hata kwenye uchaguzi ameonesha wazi anataka CCM ishinde,” alisema.

Mtatiro aliongeza kuwa, umefika wakati nafasi hizo nyeti za vyombo kama Tume ya Uchaguzi, Msajili na nyinginezo zitangazwe ili watu wenye taaluma zao washindanishwe na kuchujwa na chombo maalumu badala ya kuteuliwa na rais.

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya, alizungumzia hukumu hiyo ya Igunga akisema imetoa tafsiri mpya kwa wananchi kuelewa demokrasia ya vyama vingi na namna ya kumpata mwakilishi makini bila rushwa na vitisho.

“Hili litakuwa fundisho kwa wanasiasa wanaochezea fedha nyingi kwenye uchaguzi kununua watu, maana watatambua sasa kuwa kufanya hivyo kutawapotezea viti vyao. Lakini na wagombea wanapaswa kuwa makini na wapiga debe na vyama vyao, kwani wanaweza kuingizwa mtegoni kama alivyoponzwa Dk. Kafumu,” alisema.

Akisoma hoja zilizothibitishwa na mahakama hiyo juzi, Jaji Shangali alisema ni pamoja na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, kutumia nafasi yake ya uwaziri kutoa ahadi ya ujenzi wa daraja la Mbutu ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa Igunga.Waziri Magufuli akiwa katika uchaguzi mdogo huo katika moja ya kampeni, alitumia nafasi ya uwaziri kuwatisha wapiga kura wa jimbo hilo kuwa kama hawatamchagua mgombea wa CCM watawekwa ndani.

Jaji Shangali pia alisema kuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage, alipita mitaani akitangazia wananchi kuwa mgombea wa CHADEMA amejitoa.

Katika hoja nyingine ni kwamba Imamu Swalekh Mohamed wa Mskiti wa Ijumaa Igunga, aliwatangazia waumini wa Kiislamu kuwa wasiichague CHADEMA kwa kuwa baadhi ya viongozi wake walimdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.

Nayo matamshi ya Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, kudai kuwa CHADEMA imeleta makomandoo kuuvuruga uchaguzi huo ni mojawapo ya hoja ambazo mahakama hiyo ilizikubali.

Katika hoja kuu ya mahindi, Jaji Shangali alihoji kama wananchi wa Igunga walikuwa na njaa sana. Na kwamba, kama jibu ni ndiyo, ni kwanini uchaguzi usifanyike wakati hawana njaa.


0 comments:

Post a Comment