Meneja
wa Idara ya Habari na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP), Lilian Liundi (katikati) akifuatilia maigizo ya
wanafunzi katika hafla hiyo.
Na Thehabari.com
WANAFUNZI
mbalimbali kutoka katika baadhi ya shule za Sekondari jijini Dar es
Salaam leo wameadhimisha Siku Kuu ya Wapendanao (Valentine Day) kwa
mtanzamo wa Kijinsia ikiwa ni kushinikiza jamii kuadhimisha sherehe hiyo kwa mtazamo tofauti na mazoea kwa siku hiyo.
Wakizungumza katika
maadhimisho hayo wengi waliitaka jamii kubadili mtazamo wa maadhimisho
ya Valentine na kuijali jamii zaidi isiojiweza kwa kuisaidia kuonesha
upendo na kuacha kuegemea katika mapenzi ambayo yamekuwa yakiipotosha
jamii.
Mwanafunzi Grace David kutoka Shule ya Sekondari Loyola
alisema mapenzi ya kweli hayawezi kuoneshwa kwa mtu kwa siku moja pekee,
bali hali hiyo inapaswa kuwepo siku zote tofauti na mtazamo ya vijana
wengi wanavyoichukulia 'Valentine Day'.
Naye Meneja wa Idara ya
Habari na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania
(TGNP), Lilian Liundi akizungumza na wanafunzi alisema siku ya Valentine
hivi sasa imegeuzwa kibiashara zaidi na jamii kiasi cha kuyaathiri
makundi mengine ya jamii kwa namna mbalimbali.
Alisema takwimu
zinaonesha kuwa kadi za ujumbe wa mapenzi zinauzwa kwa kiasi kikubwa
siku hiyo ukilinganisha na sikuu kuu zingine, huku biashara nyingine za
starehe zikifanywa kiasi kikubwa.
Alisema jamii ina kila sababu
ya kuanza kubadilika na kuadhimisha siku hiyo kwa kujitolea kwa makundi
yasiojiweza kama watoto yatima, wazee na wajane ambao wanaishi katika
mazingira magumu.
Hata hivyo alisema ukatili wa kijinsia na
mapenzi umekuwa ukiibuka kwa kasi katika siku kuu hiyo; kama wapenzi
(katika ndoa) kuwasaliti wapendwa wao, ukatili wa kimapenzi, vipingo na
starehe zisizo na tija jambo ambalo linafanya makundi yasio na uwezo
kutengwa.
Aidha aliongeza kuwa wanafunzi nao wamekuwa wakijikuta
wakitoka katika maadili yao na kujiingiza katika mapenzi na ngono zembe
jambo ambalo limekuwa likiwaathiri kwa kiasi kikubwa.
"Valentine
ni maadhimisho ya kumbukumbu ya mwanaharakati aliyekuwa mtetezi wa haki
za makundi ya vijana katika jamii ya Ki-nubi ambao walinyimwa haki zao
katika masuala ya mahusiano, sasa tunaisherekea kimapenzi zaidi...,"
alisema Bi. Liundi. Makundi hayo ya wanafunzi kutoka shule za Sekondari
Yusuf Makamba, Loyola (Loyola High School), Mabibo, Perfect Vision na
Sinza Tower yamekutanishwa na TGNP kwa kushirikiana na Taasisi ya Soma
Book Cafe ya jijini Dar es Salaam. |
0 comments:
Post a Comment