Blogger Widgets

Wednesday, January 2, 2013

Huenda hiki ndicho kilichomuua Sajuki....

Imegundulika kwamba Sadick Juma Kilowoko maarufu kwa jina la Sajuki, aliyefariki dunia jana asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kumbe alipitiliza siku za kurudi kwa daktari ambapo alitakiwa kurudi hospitali India tangu tarehe 6 Desemba mwaka jana.
Hii ni kwa mujibu wa mke wa marehemu, Wastara ambaye aliwahi kumwambia mwandishi wa gazeti la Mwananchi kwamba Sajuki alipaswa kurejea India Desemba 6 mwaka jana, lakini alikwama kufanya hivyo kutokana na upungufu wa pesa. Hata hivyo alisema waliamua kuandaa matamasha mbalimbali kwa ajili ya kutunisha mfuko wa matibabu yake.

Tamasha la kwanza la wasanii hao lilifanyika mkoani Iringa Novemba 25 mwaka jana na kupambwa na wasanii wengi wa muziki na filamu. Tamasha lingine lilifanyika Desemba 18 jijini Arusha.
Sajuki ambaye hivi karibuni Serikali ilijitolea kubeba jukumu la kugharimia matibabu yake, alifariki huku akiwa akipatiwa matibabu ya awali.
Alikuwa amelazwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU), chini ya uangalizi wa karibu wa madaktari, akisubiri kusafiri kwenda India kwa mara nyingine, kuendelea na matibabu

Kabla ya kulazwa Desemba 18 mwaka jana, Sajuki alifikishwa hospitalini hapo akitokea jijini Arusha, baada ya kuanguka jukwaani kutokana na kuishiwa nguvu wakati alipopewa kipaza sauti kuwasalimia mashabiki waliofurika, ili kumtazama katika Tamasha la Asante Tanzania.

Tukio hilo lilitokea katika tamasha hilo lililohusisha wasanii wa filamu na wale wa muziki wa kizazi kipya lililofanyika ndani ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, wakati msanii huyo alipopandishwa jukwaani kuwasalimia mashabiki wake.

Baada ya kupandishwa jukwaani, alipewa kipaza sauti ili aweze kuwasalimia mashabiki wake lakini katika hali ya kawaida alifanikiwa kutamka neno moja tu,”ahhh” na kisha kudondoka akiwa juu ya jukwaa na kabla ya kutua chini, alidakwa na wasanii wenzake waliokuwa pembeni,”

Wasanii hao walimshusha jukwaani baada ya kumpumzisha kwa muda na kumtaka aende kupumzika zaidi. Akihojiwa baada ya tukio hilo, Sajuki alisema kwa sauti ya upole kwamba hali yake kiafya si nzuri kwa kuwa hana nguvu na anahitaji matibabu. ”Hali yangu si nzuri kabisa naumwa sana, sijisikii vizuri,”alisema Sajuki.

Hayo ndio maneno ya mwisho ya Sajuki kwa vyombo vya habari, wakati akiwa tayari amepitiliza siku zake za kurudi India, kuendelea na matibabu yake baada ya kukosa Sh28 milioni.

Tamasha la kwanza la wasanii hao lilifanyika mkoani Iringa Novemba 25 mwaka jana na kupambwa na wasanii wengi wa muziki na filamu. Tamasha lingine lilifanyika Desemba 18 jijini Arusha.

Ugonjwa wa Sajuki
Mwaka 2011 haukuwa mzuri kwa Sajuki kwani ndio mwaka ambao maradhi yaliyomsumbua kwa muda mrefu, yalipamba moto.

Sajuki aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa uvimbe pembeni ya ini, mapema mwaka 2011 alipoanza kuugua. Mei mwaka 2012 alifanikiwa kwenda India kwa matibabu na baadaye alirejea nchini na kuonekana kuimarika kiafya, kabla ya kuanza kuugua tena.

Kwa mujibu wa Katibu wa Chama cha Waongoza Filamu wa Wilaya ya Ilala, Rajabu Amiri, hivi karibuni, Sajuki alikuwa anasumbuliwa na tatizo la upungufu wa damu, uti wa mgongo na kansa ya ngozi.

0 comments:

Post a Comment