Blogger Widgets

Thursday, January 24, 2013

MAJAMBAZI YATEKA MAGARI ZAIDI YA MANNE NA KUWAPORA ABIRIA HUKU WAKIWAACHIA MAUMIVU MAKALI WALIOCHARAZWA VIBOKO NA MAJAMBAZI HAO

 Kwa ufupi:


Mashuhuda wameeleza kuwa majambazi hao wakiwa na silaha za kivita, waliweka kizuizi na kuyasimamisha magari hayo moja baada ya jingine kasha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi.
 
KUNDI la majambazi limeteka mabasi matano, mojawapo likiwa la wanajeshi wa Rwanda na kupora abiria na kisha kuwacharaza viboko.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi alfajiri katika Kijiji cha Kikoma kilichoko Kata ya Rusahunga, Wilaya ya Biharamulo.

Mashuhuda wameeleza kuwa majambazi hao wakiwa na silaha za kivita, waliweka kizuizi na kuyasimamisha magari hayo moja baada ya jingine kisha, kuwashusha abiria na kuwapora kila kitu.

“Baada ya kuwapora abiria, waliamua kuwacharaza viboko mmoja baada ya mwingine, kisha kutokomea kusikojulikana,” alisema shuhuda mmoja wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe na kuongeza:

“Magari yaliyotekwa ni Toyota Hiace, gari moja ni la wanajeshi waliokuwa wakitokea Rwanda kwenda Dar es Salaam.”

Diwani wa Kata ya Rusahunga, Amon Mizengo alisema tukio hilo lilihusisha majambazi wanane waliokuwa na bunduki sita za kivita.

Diwani huyo alisema magari yaliyotekwa yalikuwa yakitokea Ngara na Benaco na kuwa baada ya abiria kuporwa kila kitu, waliamuriwa kuendelea na safari zao.

Kamanda Kalangi alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi... “Ni kweli taarifa za awali zilieleza kuwa moja ya magari hayo lilikuwa na wanajeshi wa Rwanda, lakini mimi ndiyo naelekea katika eneo la tukio.”

Msemaji wa Jeshi la Wananchi nchini (JWTZ), Kanali Kapambala Mgawe alisema hana taarifa za tukio hilo wala ujio wa askari hao wa Rwanda nchini. “Sina taarifa zozote, lakini inawezekana wakawa wageni wa Kanda ya Magharibi.”

Hata hivyo, alisema katika hali ya kawaida, wageni wengi wa jeshi wanaokuja nchini, hutumia usafiri wa ndege.

Tukio hilo limetokea siku chache, baada ya wananchi wa vijiji vya mpakani wilayani Ngara, kuanza kuendesha operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu kwa kile walichodai ni Serikali kushindwa kuwasaidia.

Wananchi hao wamelalamikia wahamiaji hao haramu wenye makundi makubwa ya mifugo, kukingiwa kifua na baadhi ya viongozi wa Serikali.

Wananchi hao wa vijiji vinavyopakana na nchi za Burundi na Rwanda, kwa nguvu zao, walikamata makundi makubwa ya ng’ombe na kuwaweka chini ya ulinzi.

Katika kutuliza jazba za wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Ngara Constantine Kanyasu aliwataka wananchi kusitisha operesheni hiyo akiwaeleza kuwa Serikali inajipanga kuondoa tatizo hilo bila kukiuka sheria.

Eneo hilo limekuwa likiripotiwa matukio kadhaa ya ujambazi na mwaka 2007 wabunge wanaotokea maeneo hayo waliomba kuwekwa kwa minara ya mitandao ya simu ili kuwa na mawasiliano.

0 comments:

Post a Comment