Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam/Nairobi. Raia wa
Nigeria aliyefukuzwa Kenya miezi minne iliyopita kwa kuhusishwa na
biashara ya dawa za kulevya, amekamatwa tena nchini humo akiwa na pakiti
425 za heroin, akiaminika kwamba alipitia Tanzania.
Mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Enobemhe Emmanuel
Peter inaaminika alishukia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, Dar es Salaam, akitokea Nigeria na kisha kwenda Kenya kwa
barabara, kupitia mpaka wa Namanga mkoani Arusha.
Peter alikamatwa pamoja na mwanamke ambaye ni raia
wa Kenya, usiku wa Ijumaa iliyopita jijini Nairobi na anatarajiwa
kufikishwa mahakamani leo.
Raia huyo wa Nigeria ni kati ya wageni
waliofukuzwa nchini humo Juni mwaka huu kwa agizo la Rais wa Kenya,
Uhuru Kenyatta aliyeamuru raia wa kigeni wanaojihusisha na biashara ya
dawa za kulevya wafukuzwe nchini humo.
Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya
cha Kenya, Dk Hamisi Massa alisema uchunguzi zaidi wa dawa hizo
utafanyika kabla mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani.
“Ni kati ya watu waliokuwa wamefukuzwa nchini
katika nyumba aliyokamatiwa kulikutwa pia na pakiti 425 za heroin,”
alisema Dk Massa.
Mtu huyo amekamatwa kutokana na kuwapo kwa taarifa
zilizoonyesha kuwa, watu wengi waliofukuzwa Kenya kutokana na
kujihusisha na biashara hiyo sasa wamerejea tena.
Julai 9 mwaka huu, Ofisa Uhamiaji wa nchi hiyo,
Edward Kabiu Njau alifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa kumruhusu
Anaeke Chimenze, aliyefukuzwa nchini humo, kurejea tena.
Chimenze ambaye ni raia wa Nigeria mwenye pasi ya
kusafiria namba 02743350, pia anadaiwa kurudi nchini humo kupitia mpaka
wa Namanga.
Uhamiaji Tanzania
Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Naibu Kamishna,
Abbas Irovya alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa yupo nje ya
ofisi. “Mtafute Tatu ndiye mtu wa habari zaidi, kama atakuwa amepata
hizo taarifa atakueleza,” alisema.
Mwananchi ilipomtafuta Tatu Iddi alisema hajapata
taarifa hizo na kutaka mwandishi amtumie barua pepe ikiwa na maelezo ya
mtu huyo aliyekamatwa ili aweze kutafuta taarifa zaidi.
Naye Kaimu Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Mbaraka Batenga alisema
hayuko kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hilo kwa kuwa hakuwa
ofisini kutokana na kuugua.
Hata hivyo, alisema kwa kawaida mtu akifukuzwa kwenye nchi moja isitafsiriwe kuwa haruhusiwi kwenda nchi nyingine.
“Naomba nikusaidie kitu kimoja kama kwa ajili ya
kuelewa zaidi mambo haya, mtu akifukuzwa kwenye nchi moja haina maana
kuwa hawezi kwenda kwenye nchi nyingine, sisi tukimfukuza mtu itakuwa
kosa kama atarudi tena Tanzania,”alisema na kuongeza:
“Kwa hiyo kama huyo mtu alifanya kosa huko Kenya
na akafukuzwa Kenya ni kosa kurudi Kenya, hapo hata ofisa aliyemruhusu
kurudi huko itabidi akamatwe,” alisema Batenga.
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema mtu akifukuzwa nchi
moja haimaanishi kuwa haruhusiwi kwenda nchi nyingine.
Alisema kama kikosi cha kupambana na dawa za
kulevya cha Kenya kingekuwa kinashirikiana na kile cha Tanzania,
ingekuwa rahisi kuwadhibiti watu hao.
“Wenzetu wangekuwa wanafanya kazi kwa ushirikiano
na sisi ingesaidia sana, wakimkamata mtu wanatuambia. Huyo mtu alipita
tu Tanzania,” aliongeza Nzowa.
Nzowa alitahadharisha kuwa kumfukuza sio kigezo cha kumzuia mtu kupita Tanzani
0 comments:
Post a Comment