Johannesburg.
Mtanzania Agnes Gerald, maarufu Masogange, ameachiwa huru na Mahakama
ya Kempton ya jijini Johannesburg, baada ya kulipa faini ya R30,000
(Sh4.8 milioni) kwa kosa la kubeba kemikali zinazotumika kutengeneza
dawa za kulevya
Wakati
Masogange akitozwa faini hiyo mwenzake, Melissa Edward ameachiwa huru na
mahakama hiyo, baada ya kukosekana ushahidi wa kumtia hatiani.
Msemaji wa
Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai cha Afrika Kusini(Hawk),
Kapteni Paul Ramaloko alisema Watanzania hao wameachiwa huru baada ya
kuonekana kuwa hawakubeba dawa za kulevya, bali kemikali aina ya
ephedrine.
Hata
hivyo, Mahakama ilibaini kuwa, Melissa hana hatia kwa kuwa ilionekana
kuwa amemsindikiza Masogange, ambaye alimwomba amsaidie kubeba mzigo
huo.
"Mahakama
iliona kuwa Melissa aliombwa tu kumsaidia kubeba baadhi ya mabegi,
lakini hayakuwa yake. Mizigo yote iliandikwa jina la Agness Gerald na si
Melissa," alisema Kapteni Ramaloko.
Kapteni
Ramaloko alisema, Melissa alijitetea kuwa hakuwa amesafiri pamoja na
Masogange bali walikutana ndani ya ndege na Masogange alimwomba amsaidie
kubeba mizigo hiyo, kwani ilikuwa mikubwa.
Kwa
sheria za Afrika Kusini kubeba kemikali zozote ambazo zimepigwa marufuku
ni kosa la jinai kisheria, hivyo mahakama iliamuru Masogange ahukumiwe
kwenda jela kwa miezi 30 (miaka miwili na miezi mitano) au alipe faini
ya R30, 000 (sawa na Sh4.8 milioni).
Hata hivyo, Kapteni Ramaloko alisema mdhamini wa Masogange alilipa nusu ya fedha na kwamba zinazobaki amalizie baadaye.
Alisema
kutokana na kutomalizia kulipa fedha hizo ataendelea kubaki nchini humo
hadi atakapomaliza kulipa nusu ya faini iliyobaki.
Masogange na mwenzake walipokamatwa na SARS ilielezwa walikuwa wamebeba dawa za kulevya aina ya
Methamphetamine, lakini Mahakama juzi ilithibitisha walikamatwa na kemikali aina ya Ephedrine, ambayo siyo dawa za kulevya.
Wakati
Kamishna Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini, Geofrey
Nzowa alipoulizwa na Mwananchi Jumamosi juzi alisema mzigo walioubeba
Masogange na mwenzake haukuwa ni dawa za kulevya bali ni kemikali za
dawa za kulevya, lakini Msemaji wa Mamlaka ya Mapato ya Afrika Kusini,
(SARS), Marika Muller alieleza kuwa timu ya SARS ina uhakika kuwa mabegi
sita yaliyokamatwa Julai 5 ni dawa za kulevya aina ya
Methamphetamine.Jana, Muller alipoambiwa kuwa Watanzania hao wameachiwa
huru baada ya kulipa faini na mmoja kuachiwa huru kwa kuwa Mahakama
imeridhika kuwa hazikuwa methamphetamine bali kemikali aina ya
Ephedrine, alirudia tena na kueleza kuwa, mamlaka hiyo ina uhakika na
kazi yake na iwapo mahakama imewaachia huru basi yeye hana la kusema
zaidi.
"Kazi
yetu kubwa ni kukamata mizigo haramu inayopitishwa uwanja wa ndege, kama
Mahakama imeona kuwa si dawa za kulevya, hatuna la kuongeza. Kikubwa
tumemaliza kazi yetu," alisema Muller kwa kujiamini.
Hata
hivyo, Nzowa jana akizungumzia kuachiwa huru kwa Watanzania hao,
alionyesha kushangazwa jinsi Mahakama ilivyotoa adhabu ndogo.
"Hii ni
ajabu sana. Kama watu wamebeba mzigo wenye thamani ya Sh6.8 bilioni
wanapigwa faini ya milioni nne, hawataogopa kufanya hiyo biashara. Hao
watu ni hatari sana," alisema Nzowa.
Alipoulizwa
iwapo wakirudi Tanzania wanaweza kushtakiwa, Nzowa alisema kitengo
chake hakitaweza kuwashtaki tena kwa sababu wanaweza kujitetea kuwa
tayari walishahukumiwa, isipokuwa Mwendesha Mashtaka aliyekuwa
akisimamia kesi yao anaweza kukata rufaa.
"Iwapo
Mwendesha Mashtaka wa huko akikata rufaa kwa kuona adhabu aliyopewa
mhalifu huyo ni ndogo, anaweza kufanya hivyo," alisema Nzowa.
Nzowa alisema, inasikitisha kuwa wakati mapambano ya biashara hiyo yakiwa yanaendelea Tanzania, watuhumiwa hao wanaachiwa.
"Adhabu
waliyopewa ni ndogo hasa wakati huu ambao Tanzania tunachafuka kwa
tuhuma hizi. Lazima kitu kifanyike kubadili hali halisi hapa nchini,"
alisema.
Nzowa
alieleza kuwa alikwenda Afrika Kusini tangu Septemba Mosi kuwahoji
wasichana hao ambao hata hivyo hawakuweza kusema lolote la kuisaidia
polisi.
Masogange
aliandika kwa maandishi kuwa ni kweli mzigo ulikuwa wa kwake, lakini
akasema mdogo wake, ambaye ni Melissa, hajui lolote na alikuwa
amemsaidia.
Julai 5,
mwaka huu Masogange na Melissa walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Oliver Tambo wakidaiwa wamebeba kilo 150 zilizodaiwa kuwa
ni dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye thamani ya Sh6.8
bilioni.
Dawa hizo
zilizokuwa zimepakiwa katika mabegi makubwa sita, zinatajwa kuwa ni
kiwango kikubwa kukamatwa katika historia ya SARS ndani ya uwanja huo
unaotumiwa na mataifa makubwa duniani.Taarifa za kukamatwa kwa wasichana
hao zilipamba kurasa mbalimbali za magazeti ndani na nje ya Tanzania,
jambo lililosababisha Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kuchukua
hatua za kuusafisha Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
Baada ya
uchunguzi wa Dk Mwakyembe ambao ulibaini kuwapo mchezo mzima uliochezwa
wakati Masogange na Melissa walipokuwa uwanja wa ndege.
Agosti 17
alitoa agizo la kufukuzwa kazi, Koplo Juliana Thadei, Jackson Manyoni,
Yusuph Daniel Issa, Koplo Ernest na Mohamed Kalugwan.
Mwakyembe
alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida mfanyabiashara ambaye hakuwa
na tiketi ya kusafiri siku hiyo, baadaye alibadili mawazo hapohapo na
kuamua kuondoka siku hiyo kwenda Afrika Kusini na kulipia faini ya dola
60 (Sh96, 000) ili kupata tiketi.
Pia
Mwakyembe aliliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na Polisi wa Kimataifa
(Interpol) kumkamata mfanyabiashara anayedaiwa kumsaidia Masogange
kusafirisha dawa za kulevya ambaye alitoweka na mabegi matatu ya dawa
hizo huko Afrika Kusini:
chanzo mwananchi.
0 comments:
Post a Comment