Blogger Widgets

Thursday, September 5, 2013

INATISHA: DAKITARI AFUMANIWA AKIWA KWENYE JARIBIO LAKUMTOA MIMBA MWANAMKE, ZAIDI SOMA HAPA

AMA kweli hii bombastiki! Daktari Afrika Kweka amenaswa katika Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’ akiwa katika jaribio la kumtoa mimba mwanamke aliyejulikana kwa jina moja la Stella.
Tukio hilo lilitokea juzikati kwenye chumba kilichopo katika jengo la Chama cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Makurumla, Magomeni-Kagera, Dar.
Awali, raia wema wa eneo hilo walituma malalamiko yao kwa OFM wakidai kwamba, Dokta Kweka amekuwa akifanya ‘mauaji’ hayo ya vichanga waziwazi, hali inayowakera kupita maelezo.
“Jamani ninyi si ndiyo Oparesheni Fichua Maovu? Kwa taarifa yenu hapa Magomeni-Kagera kwenye jengo la CCM, Tawi la Makurumla, kuna daktari anaitwa Kweka anatoa sana mimba, hasa wake za watu, njooni mumnase.”
 Baada ya kupata taarifa hiyo, OFM ilipanga mtego ambapo mmoja wa waandishi wetu wa kike alikwenda kwa Dokta Kweka na kujifanya mwanafunzi wa chuo lakini ana mimba anataka kuichoropoa.
Dk. Kweka.
Mwandishi huyo aliingia na paparazi wa kiume aliyejifanya ni mpenzi wake aliyempa mimba hiyo. Ndani ya eneo la tukio walipokelewa kwa bashasha na daktari huyo ambaye alihitaji shilingi 60,000 kama gharama za kutoa mimba japo baadaye alikubali kushusha bei hadi shilingi 45,000.
Vifaa anavyotumia Dk. Kweka.
Baadaye daktari huyo alimchukua mwandishi wetu bila kujua kama hakuwa na mimba wala kitambi na kumpeleka chumba cha kuchomea sindano ambapo almanusura mpango mzima uharibike kwa kuwa mwandishi wetu hakupaswa kuruhusu daktari huyo amchome sindano ambayo ilisadikika kuwa ni ya ganzi.
Hata hivyo, wakati paparazi wetu akijishauri kuhusu sindano hiyo, ndipo Stella alifika kwenye zahanati hiyo na kuingia ndani kwa dhumuni la kutoa mimba.
Alipofika aliingia moja kwa moja chumbani kwa daktari huyo na kuchoma sindano ya ganzi bila woga kisha akaingia chumba cha kuchoropolea.
Vifaa vinavyotumika kuchoropoa mimba.
OFM ilipata uhakika kuwa, mwanamke huyo ameingia chumba cha kutolea mimba, ndipo ‘wapenzi’ hao (mapaparazi wetu) waliwasiliana na wapiga picha wetu waliokuwa chobingo na polisi ambao walitia timu na kuwanasa.
Daktari huyo na mteja wake walipelekwa kituo cha polisi na kufunguliwa jalada la kesi namba MMP/RB/567/2013 kosa likiwa kujaribu kutoa mimba huku ikibainika kuwa zahanati hiyo ni batili kwa kuwa aliisajili kama maabara.
Naye Katibu Mwenezi wa CCM wa tawi hilo, Hashim Kimambe alizungumza na gazeti hili juzi na kukiri kuwa taarifa za kunaswa kwa daktari Kweka anazo.
Alisema: “Hata hivyo, sisi tulikuwa mbioni kumfukuza kwa sababu alipoomba kupanga hapa alisema anaweka duka la dawa (famasi), baadaye tukashangaa anaziba watu wanaingia ndani.
“Mbaya zaidi huyu jamaa amekuwa akitumia risiti za CCM katika mambo yake, lazima aondoke kwa kweli, tunamwandikia barua.”
Imeandaliwa na Chande Abdallah, Denis Mtima, Mayasa Mariwata, Issa Mnally, Richard Bukos na Hamida Hassan.

0 comments:

Post a Comment