11:12 AM
11/03/2013 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SALAAM,
JANA na leo, zimetolewa habari tofauti kuhusiana na kalbu ya Simba
ambazo uongozi umeona ni vema uzitolee ufafanuzi kwa lengo la kuweka
rekodi sawa. Ufuatao ndiyo ufafanuzi wa taarifa hizo.
1. SIMBA KUZUIWA HOTELINI
SAA mbili kabla ya mechi ya jana baina ya Simba na Coastal Union ya
Tanga, mmiliki wa Saphire Court Hotel alitoa taarifa kwa uongozi wa
Simba kwamba ataizuia timu isiondoke hotelini kwa vile anaidai Sh
milioni 25 na anataka alipwe zote jana.
Ikumbukwe kwamba Simba
imekuwa ikikaa hotelini hapo kwa muda mrefu sasa wakati inapoweka kambi.
Pia, wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba walifanya mkutano na
wachezaji wote wa Simba katika hoteli hiyo usiku wa kuamkia jana.
Wamiliki wa hoteli hiyo hawakutoa taarifa yoyote kwa uongozi wakati huo
juu ya dhamira yao hiyo.Wamiliki hao hawakutoa taarifa asubuhi ya mechi
na walisubiri mpaka wakati timu inataka kuondoka ndiyo wakachukua hatua
hiyo.
Kwa uongozi wa Simba, hatua hiyo ilikuwa ya ghafla mno.
Ifahamike kwamba kabla ya hatua hiyo, uongozi wa Simba ulikuwa umemlipa
mmiliki huyo kiasi cha zaidi ya Sh milioni 30 katika kipindi cha miezi
10 iliyopita.
Mara baada ya mechi dhidi ya Libolo ya Angola,
Saphire walilipwa Sh milioni 15 na Simba. Hii maana yake ni kwamba klabu
yetu ina utaratibu wa kulipa madeni yake na si watu wasiolipa kama
hatua hiyo ya wamiliki wa Saphire inavyotaka kueleza.
Uongozi
wa Simba tayari ulitoa ahadi ya kumaliza deni lote inalodaiwa baada ya
kulipwa fedha zake inazodai zinazotakiwa kulipwa wakati wowote mwezi huu
au ujao. Simba inadai zaidi ya Sh milioni 500 kwa wadai wake wawili
(Etoile du Sahel ya Tunisia na Push Mobile) na inataraji kulipwa fedha
hizo.
Itakapolipwa fedha zake hizo, Simba itakuwa na uwezo wa
kulipa madeni yake yote inayodaiwa na watu binafsi na makampuni bado
ikabaki na fedha za kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.
Wakati ikisubiri ilipwe fedha zake inazodai, Simba itaendelea kulipa
madeni yake taratibu kwa kadri itakavyoweza. Ifahamike kwamba kwa sasa
chanzo kikuu cha mapato ya klabu ni fedha za mapato ya milangoni na za
udhamini wa bia ya KILIMANJARO ambazo hazikidhi mahitaji yote ya timu.
Kwa kuzingatia nakisi hii ya mapato na matumizi, Simba SC imeanza
mchakato wa kutafuta wafadhili na wadhamini kokote walipo duniani ili
kuongeza mapato yake. Tayari mawasiliano yameanza na wenzetu wa
Sunderland ya England kupitia mradi wao wa Invest in Africa ili Simba
nayo ifaidike.
Simba SC inaomba pia umma ufahamishwe kwamba
klabu ya soka kudaiwa si dhambi. Iwapo klabu kubwa na tajiri duniani
kama vile Manchenster United, Real Madrid na Liverpool zina madeni,
inakuaje madeni ya Wekundu wa Msimbazi (tena ambayo klabu ingeweza
kuyalipa yote iwapo wadeni wake nayo wangewalipa kwa wakati) yaonekane
kama kitu kigeni?
Uongozi unaahidi kwamba utalipa madeni yake
yote kwa kadri utakavyojaaliwa. Kwenye lugha ya kibenki, credit
worthiness ya mteja inamaanisha mteja ambaye anakopa na kulipa. Simba
inapenda kusisitiza kwamba ni taasisi ya kuaminika na yenye heshima
kubwa na bado inavutia watu na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya
nchi.
Hata hivyo, uongozi wa Simba unafikiria kuchukua hatua za
kisheria dhidi ya wamiliki wa Saphire Court Hotel kwa kitendo chake cha
kuwazuia wachezaji na viongozi wa Simba hotelini kabla ya mechi ya
jana.
Simba inachukulia kitendo kile kama hujuma na kisheria
kinaangukia katika kundi la Forced Imprisonment, kwa mmiliki kuwazuia
watu kinguvu. WAMILIKI hawakutoa notisi kwa uongozi au taarifa yoyote ya
mdomo au maandishi kabla ya kuchukua hatua hiyo.
Lengo
lilikuwa ni kuchafua heshima na hadhi ya Simba kwa hoteli ambayo imetoka
kulipwa Sh. milioni 15 wiki mbili tu zilizopita. Uongozi wa Simba SC
unaapa kuilinda na kuitetea hadhi ya klabu yetu kwa nguvu zetu zote,
akili zetu zote na maarifa yetu yote.
2. WACHEZAJI, BENCHI LA UFUNDI KUFUKUZWA
KUNA taarifa zimeenezwa pia kwamba kuna wachezaji wa Simba
wamesimamishwa au kufukuzwa kuchezea Simba. Habari hizi nazo hazina
ukweli wowote
Ukweli ni kwamba, uongozi wa Simba umetoa ruksa
kwa benchi la ufundi kupanga timu ambayo litaona inafaa kwa mechi
husika. Uongozi hautaingilia, kwa namna,njia au aina yoyote ile utendaji
wa benchi la ufundi.
Hakuna mchezaji yeyote aliyesimamishwa
hadi sasa. Pia uongozi unakanusha taarifa kuwa Daktari Mkuu wa Klabu,
Cosmas Alex Kapinga, kuwa naye ameachia ngazi. Habari hizi hazina ukweli
kwani daktari huyo ana ruhusa ya kikazi ya wiki mbili inayojulikana.
HITIMISHO
KATIKA namna ya kipekee kabisa, uongozi wa Simba unapenda kutoa
shukrani za dhati kabisa kwa washabiki wake waliojitokeza Uwanja wa
Taifa na kuisapoti timu kwa asilimia 100. Uongozi unathamini sana
mchango wa wanachama wake na unaahidi kufanya kila unachoweza
kuwarejeshea tena furaha mioyoni mwao.
Uongozi pia unatumia
nafasi hii kuwapongeza wachezaji na benchi la ufundi ambao walicheza
mechi ya jana katika mazingira magumu. Walicheza bila ya kufanya warm up
na wakitoka kuwa wamezuiwa hotelini jambo ambalo lingeweza kuwaondoa
mchezoni.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
SIMBA SC
0 comments:
Post a Comment