"SIRI YA KUUAWA ZITTO’
Katika gazeti la Mtanzania toleo na. 7269 la Jumatano Machi 27, 2013 kuna habari yenye kichwa chenye maneno ‘ SIRI YA KUUAWA ZITTO YAFICHUKA’ na
vichwa vidogo ‘yadaiwa ilipangwa anyweshwe sumu hotelini’ dk. Slaa
atajwa kumtuma Saanane kummaliza’. Habari hii imeniletea usumbufu mkubwa
kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wangu, wamejazwa na
wasiwasi mkubwa sana kwamba ninaweza kuuwawa. Napenda kusema yafuatayo:
Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben
Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na
akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time
ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi. Haijawahi
kutokea mimi kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na
Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika na hivyo
naomba mwandishi ahakikishe kuwa vyanzo vyake vya habari vimempa habari
sahihi.
Pili, Siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu anaweza kupanga
kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba
mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti. Kila mtu atakufa. Kama
nitakufa kwa kuuwawa na mtu mwingine ndio itakuwa nimeandikiwa hivyo na
Mungu. Ndio maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuwawa
nk. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndio furaha ya maisha
yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili lakini
mawazo, fikra na maono ya Zitto yataishi tu. Siogopi kufa maana maisha
niliyoyachagua ndio haya ambayo yamejaa vitisho. Muhimu kwangu ni
kufanya kazi zangu kwa bidii, uhodari na uaminifu. Siku zote nitasimamia
ukweli bila kujali uchungu wa ukweli huo.
Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine
watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia
masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena. Kama mtu kaamua kuhama
CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA maana kama
angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye
anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa. CHADEMA sio
pango la watesaji wala wauaji. Kama kuna mwanachama wa chama kingine
cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu
aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki. Matendo ya mtu mmoja
yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi.
Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu
kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk
kamwe havijengi chama. Chama chetu lazima kiwe mfano bora wa kuheshimu
demokrasia na haki za binaadamu. Wananchi hawawezi kutoa dola kwa chama
chenye mifarakano. Tusiruhusu kugawanywa kwa matakwa ya watu wachache.
Tusimamie misingi ya kuanzishwa chama chetu.
0 comments:
Post a Comment