Blogger Widgets

Sunday, June 9, 2013

KIFO CHA ALBERT MANGWEA – HIVI UNADHANI KIFO CHAKE KINATUULIZA MASWALI GANI ?.


Albert Mangwair PerformingNa Freddy Macha.
BABU wa fasihi ya Kiswahili, Shaaban Robert alifariki mwezi huu mwaka 1962. Ingetakiwa sikukuu ya kifo chake yaani Juni 20 ifanyiwe maadhimisho kila mwaka. Sisi na wenzangu wa Bendi ya Sayari tuliwahi kusheherekea kwa maonyesho ya 1983. Hazina hii tukufu ya taifa inatakiwa zaidi ya hilo.

Moja ya vitabu vyake babu ni “Kielezo cha Fasili” kilitolewa upya na mwongozi wa wachapishaji Tanzania; “Mkuki na Nyota” ,2004 na kinafafanua mashairi yake kwa wasomaji mintaarafu ya kujenga mapafu kilugha.

Ananyambua Shairi la “Jina”: “Mwanadamu mwenye fikra njema huacha fahari au sifa kwa wat
u ambayo vizazi vyake vya nyuma yake hupenda kuiona na ambayo itakuwa kama hazina kwa watu wote katika dunia.”

Albert Mangwea hakuwa Shaaban Robert; amefariki akiwa na miaka 31 tu. Lakini Mangwea au Mangair alitumia fani ya ushairi kuchangia kuiendeleza fasihi ya Kiswahili na kipaji chake alichomegewa na Muumba.

Kifo hiki kilichokua Usauzi (Afrika Kusini) kimezungumziwa na kinaendelea kuzungumziwa. Mwaka jana wakati kama huu, Tanzania ilimpoteza Steve Kanumba. Vifo vya chipukizi hawa vimeacha utata na mijadala marefu.

Mangwea alifia ughaibuni. 
Maisha ugenini ni magumu maana habari huwa hazitangazwi sana. Mbali na taratibu za kisheria, kinachongojewa kutufariji huwa viongozi wa dini na Serikali.

Vipo vifo vya aina nyingi. Ila vifo vinapokuwa na utata husubiri mkono wa sheria utubembeleze. Kanumba alifuatiliwa na mashtaka ya msichana aliyekuwa naye; Mangwea, hatuyajui bado kiuhakika...

Miaka iliyopita habari za vifo vya Waafrika hasa zile zilizohusiana na Ukimwi au dawa za kulevya hazikuwekwa wazi, sababu ya aibu, miiko na staha. Nakumbuka wanamuziki wawili maarufu Hukwe Zawose na mpwa wake, Charles Zawose walipofariki, wanahabari hatukueleza chanzo ili kuheshimu hisia za familia zao.

Magazeti ya ughaibuni, walakini, hayakupepesa.

Mwanamuziki Charles Zawose alifariki ghafla akijitayarisha kupanda ndege Sweden alikokuwa akifanya maonyesho ya muziki wa kijadi, 2004. Kwa kuwa Charles na baba yake mkubwa walishajenga majina ugenini habari zilichambuliwa katika magazeti viongozi. Mwandishi John Lusk wa “Independent” gazeti linaloheshimika sana Uingereza aliandika:

“Kifo kimenyamazisha moja ya himaya kubwa ya familia ya wanamuziki wa Tanzania... Walikuwa mabalozi viongozi wa muziki wa Kigogo.” Akaongeza kuwa Zawose amefariki kutokana na “maradhi yaliyosababishwa na Ukimwi.”

Nyumbani, lakini, ugonjwa haukutajwa.
CHANZO MWANANCHI.

0 comments:

Post a Comment