Blogger Widgets

Tuesday, July 23, 2013

KODI YA SIMU BALAA...!!! EM SOMA HAPA

MOTO wa tozo mpya ya kadi ya simu ya sh 1,000 kwa mwezi, unazidi kukielemea Chama cha Mapinduzi.
Wakati viongozi waandamizi wa CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, akitoa msimamo wa kuitaka serikali kusitisha uamuzi wa tozo hiyo, huku Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Mizengo Pinda, akiponda waziwazi kauli hiyo, mbunge wa Ubungo, John Mnyika, ameibuka na kudai kuwa hiyo ni
ishara ya wazi kuwa serikali inayumba.
Wiki hii Pinda alisema kuwa wanaopinga kodi hiyo hawana jema, kwa kuwa tozo hiyo sio ya kuwaumiza wananchi bali mapato yake yatakwenda moja kwa moja kusaidia kueneza umeme vijijini.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano jana Mnyika (CHADEMA), alisema kutokana na kusigana kwa viongozi hao ni muhimu Rais Jakaya Kikwete kwa nafasi yake anapaswa kuziba ombwe la uongozi lililopo na kutoa mwelekeo kwa maslahi ya wananchi.
Alisema kuwa ni vizuri Pinda akajieleze au ajiuzulu kutokana na kauli yake na viongozi wenzake kutofautiana.
“Kauli hii ni tofauti na maelezo yake na ya wenzake katika mkutano uliomalizika bungeni ambapo ilielezwa kwamba serikali inaanzisha tozo mpya ya mafuta ya petrol (petroleum levy) ya sh 50 kwa lita na mapato yake yatagharamia mahitaji ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA),” alisema.
Alisema kuwa wakati Waziri Mkuu Pinda akisema hayo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa, alisema kwamba serikali inaendelea kupokea maoni kwa wadau na wananchi kwa ajili ya kurekebisha kodi hiyo.
Huku Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Makame Mbarawa akikaririwa akizungumzia ushuru huo na kusema kuwa serikali itahakikisha wananchi hawabebeshwi mzigo usiokuwa na sababu.
Mnyika alionyesha kutofautiana kwingine ni kwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo January Makamba ambaye alisema kwamba wizara yao ilipinga kodi hiyo tangu awali na kupita kwake ilikuwa ni kutokana na kuzidiwa nguvu na kwamba haliwezi kutekelezeka.
Alisema kuwa Baraza la mawaziri linaongozwa na misingi ya uwajibikaji wa pamoja hivyo kwa utata wa kauli hizo zinazopingana, ni wazi hakuna kauli moja ya serikali.
“Rais Kikwete anapaswa kushughulikia udhaifu huo kwa kutoa msimamo wenye mwelekeo wa serikali kuwasilisha bungeni muswada kwa hati ya haraka kufuta kodi hiyo na kupendekeza vyanzo mbadala vya kuziba pengo kuhakikisha miradi ya maendeleo.”
Alisema Waziri Mkuu Pinda anapaswa kueleza iwapo wananchi wana sababu ya kuendelea kuwa na imani naye katika mazingira haya ya serikali kutoa maelezo tofauti bungeni na nje ya Bunge.
Alisema Pinda ndiye mwenye mamlaka na madaraka ya udhibiti, usimamiaji na utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za serikali anapaswa kueleza sababu za yeye na mawaziri wake kutofautiana hadharani na ni kwa nini wasijiuzulu na baraza la mawaziri livunjwe.
Alisema kuwa kwa madaraka ya Rais ibara ya 33 ya Katiba ya nchi na watumishi wote wa serikali kwa mujibu wa ibara ya 35 wanafanya kazi kwa niaba yake anapaswa kutumia mamlaka yake, anayo haki ya kuwaondolea mzigo huo mwingine usiokuwa wa lazima wa gharama za maisha wananchi.
“Ubovu wa Katiba ya nchi ibara ya 99 umetoa mwanya wa mamlaka makubwa kuwa kwa Rais kuhusu kutoza kodi au kubadilisha kodi ambapo imeelekezwa wazi kwamba Bunge haliwezi kushughulikia masuala hayo isipokuwa kupunguza mpaka Rais awe amependekeza kwamba jambo hilo lishughulikiwe na Bunge na pendekezo hilo la Rais liwe limewasilishwa kwenye Bunge na waziri,” alisema.
“Rais Kikwete atoe msimamo wa kuwasilisha muswada kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi,” alisema.
Alisema kuwa Rais Kikwete afanye hivyo kwa kuwa serikali kupitia mipango yake na ilani ya uchaguzi ya chama hicho iliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania kuanzia mwaka 2005 lakini tangu wakati huo kumekuwa na maisha magumu kwa wananchi walio wengi.
Mnyika alisema kuwa kuwepo kwa udhaifu katika uzalishaji, usambazaji wa bidhaa muhimu nchini, soko ‘holela’ na ongezeko la uagizaji wa bidhaa kutoka nje, hali hii inachangiwa pia na ongezeko la kila mwaka la kodi.
Alisema kuwa katika bidhaa na huduma zinazotumiwa na wananchi walio wengi, serikali inapaswa kupanua wigo wa vyanzo mbadala vya mapato.
“Hali hii ilianza hata kabla ya kupitishwa kwa muswada wa Sheria ya Fedha Juni 28, ya mwaka huu ambao ulisainiwa na Rais Kikwete kwa ajili ya kuanza kutumika Julai 1, 2013,” alisema.
Alisema kuwa malalamiko ya muda mrefu ya wananchi ni namna walivyosaini fomu za madai ya kutaka Bunge liingilie kati kuisimamia serikali kudhibiti na kupunguza athari za ongezeko bei na gharama za maisha.
“Kabla ya kuanza kwa mkutano wa 11 wa Bunge Aprili 8, 2013 nilikuwa tayari nimepokea orodha ya watu waliosaini fomu zaidi ya 18,000 na niliwasilisha taarifa ya ombi hilo la wananchi, hata hivyo halikuweza kujibiwa kwa ajili ya kujadiliwa bungeni kwa kuwa mkutano huo ratiba yake ilijikita katika Bajeti ya Serikali,” alisema.
Serikali ilipaswa kusoma alama za nyakati na kuitumia bajeti ya mwaka 2013/2014 na muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2013 kama zana ya kutekeleza dhana ya kupunguza gharama za maisha kwa wananchi kwa kuweka mkazo sio tu kwenye miradi ya maendeleo ya kuongeza uzalishaji.
Alisema kuwa badala ya kuchukua hatua hiyo serikali ikaendeleza kuongeza kodi kwa sehemu kubwa kwa vyanzo vile vile na vingine vyenye kuwalenga wananchi walio wengi.
“Katika hali hiyo ambayo ilinifanya kwenye mchango wangu bungeni Juni 27, 2013 niuite muswada wa sheria ya fedha kuwa ni ‘muswada wa majanga’ wenye kuongeza gharama za maisha ya wananchi kutokana na ongezeko kubwa la kodi kwenye simu na mafuta,” alisema.
Alisema hayo alipozungumza kwenye mkutano wa hadhara mjini Songea juzi, katika ziara yake ya wiki moja mkoani Ruvuma.
Pinda alisema, “Ni kama vile tozo iliyoongezwa kwenye mafuta ya petroli, ambayo imetupa fedha nyingi katika mfuko wa barabara za kuunganisha miji na mikoa.”
Aliongeza: “Nani asiyetaka vijiji vipate umeme kama miji, ili usaidie kuondoa giza, uendeshe viwanda vidogo vidogo na usaidie kukuza uchumi? Wanaopinga tozo hii, hawatutakii mema,” alisema Pinda.

TANZANIA DAIMA

0 comments:

Post a Comment