Blogger Widgets

Wednesday, July 31, 2013

SERIKALI YAFANYA UPYA UTAFITI KUHUSU MAFUTA YA UBUYU


Moja ya aina za bidhaa za mafuta ya ubuyu.
Utata wa kauli kuhusu usalama wa mafuta ya ubuyu, umesababisha Serikali kuyafanyia utafiti na hivi karibuni itatoa tamko la kumaliza gumzo hilo.


Akizungumza na mwandishi jana kuhusu utata huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando, alisema Serikali iko katika hatua za mwisho za utafiti huo, na muda si mrefu itatoa msimamo ili kuondolea wananchi utata.
“Tumeona kila mtu anazungumzia usalama wa mafuta ya ubuyu, lakini siku chache zijazo tutawaita na kutoa msimamo wa Serikali ili kuwaondolea wananchi utata uliopo wa kila mtu kusema lake,” alisema Dk Mmbando.
Utata kuhusu usalama wa mafuta ya ubuyu, ulianza mwezi uliopita baada ya Taasisi ya Chakula na Dawa (TFDA), kueleza kuwa mafuta hayo si salama kunywewa, kwani yana tindikali inayosababisha saratani.
Kauli ya TFDA, iliungwa mkono na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,  iliyoweka wazi kuwa haitambui mbegu za ubuyu kuwa zinatoa mafuta ya tiba, isipokuwa inatambua tiba inayotokana na mti huo ni majani, magome na unga.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili na Mbadala wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Paulo Mhame, alisema Serikali haitambui mafuta ya ubuyu kama tiba.
Hata hivyo, mwanzoni mwa wiki hii, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ilitangaza kuwa mafuta hayo ni salama  yakitumiwa vizuri.
Daktari Bingwa wa Udhibiti wa Saratani wa taasisi hiyo, Dk Crispin Kahesa, alinukuliwa akisema hadi sasa hakuna utafiti wowote wa kitaalamu, uliopata kufanywa na kuonesha kuwa mafuta hayo ni chanzo cha saratani ya ini.
“Mafuta ya ubuyu si dawa bali yanazuia maradhi sugu yasiyoambukiza, ikiwamo saratani kwa sababu kitaalamu yana ‘anti oxidant’ (uchachu) ambayo pia hupatikana kwenye baadhi ya matunda kama maembe, machungwa na mananasi.
“Tofauti iliyopo, ni kwamba mafuta hayo yana anti oxidant nyingi tofauti na iliyomo kwenye matunda. Anti oxidant husaidia kukinga maradhi ambayo mengi si ya kuambukiza - maradhi sugu kama vile saratani, kisukari na shinikizo la damu,” alikaririwa Dk Kahesa.
Kazi nyingine ya anti oxidant mwilini ilitajwa kuwa ni kuondoa sumu na kusaidia kutengeneza chembechembe hai mwilini. 
“Narudia, mafuta ya ubuyu hayana madhara yakitumika vizuri, bali madhara ambayo watu wanayasema, yanatokana na jinsi wanavyoyatumia, kwani wajasiriamali wanaoyatoa hawajui ni mgonjwa gani anapaswa kuyatumia na kwa wakati gani,” alikaririwa Dk Kahesa.
Kutokana na tamko hilo,  wiki hii pia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, jana alitangaza kuwa mafuta hayo si salama na kusisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Serikali, hivyo wananchi waamue kuyatumia au kutoyatumia.
Dk Rashid alitoa kauli hiyo kujibu maswali ya waandishi wa habari baada ya kufungua semina ya siku mbili, iliyoandaliwa na  TFDA na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Tayari chombo cha Serikali ambacho kina mamlaka juu ya hili kimeshatoa tamko, hivyo ni hiari ya wananchi kuamua kuyatumia au kuacha.
“Kwa sababu ni sawa na sigara, tumesema kabisa sigara inasababisha saratani na matatizo mengine, tukaweka na onyo kwenye kasha la sigara, hivyo ni hiari kutumia au kutotumia,” alisema.

0 comments:

Post a Comment