Blogger Widgets

Wednesday, May 15, 2013

MAAJABU: ANGELINA JOLIE AAMUA KUONDOA MATITI YAKE YOTE MAWILI NA KUNG'OA KIZAZI KWA UPASUAJI!!



Mcheza sinema maarufu wa Kimarekani, Angelina Jolie, ametangaza kwamba amefanyiwa operesheni ya kuondosha matiti yake yote mawili ili kupunguza uwezekano wa kupata saratani ya maziwa na ya kizazi. 

Kwa mujibu wa makala yake iliyochapishwa leo kwenye gazeti la The New York Times na kupewa jina "Chaguo langu la kitabibu", Angelina Jolie amesema ameamua kutangaza jambo hilo hadharani ili kuwapa moyo wanawake wengine wenye historia ya familia zinazouguwa saratani.

Mama yake mwenyewe Angelina alifariki akiwa na miaka 56 kutokana na maradhi hayo. Sasa muigizaji huyo maarufu wa sinema duniani, anasema anawataka wanawake wenye hali kama yake kutafuta ushauri wa kitabibu na kufanya uamuzi baada ya kuwa na taarifa za kutosha ili waweze kuendelea kufanya kazi, kama alivyofanya yeye.

"Licha ya kuweza kulifanikisha hili na kubakia kimya kwa muda mrefu, sasa naandika kulitangaza kwa sababu natarajia kuwa wanawake wengine wanaweza kufaidika na uzoefu wangu." Ameandika mjumbe huyo maalum wa Umoja wa Mataifa juu ya masuala ya wakimbizi.
Uamuzi mgumu lakini muhimu 
Jolie aliamua kufikia uamuzi huo wa kuyaondosha matiti yake yote mawili, kwa sababu alifahamishwa na madaktari wake kwamba alikuwa na chembechembe inayoongeza hatari ya kupata saratani kwenye maziwa yote mawili na kwenye fuko lake la uzazi.

Kutokana na chembechembe hiyo iitwayo BRCA1, madaktari walikisia kwamba alikuwa kwenye kiwango cha asilimia 87 ya hatari ya kupata saratani ya maziwa na asilmia 50 ya kupata saratani ya kizazi.

"Baada tu kujua kwamba huo ndio ukweli kuhusu hali yangu, niliamua kuchukua hatua za kabla na angalau kupunguza kiwango hicho cha hatari kadiri nilivyoweza. Nikafanya uamuzi wa kuondosha matiti yangu yote mawili. Nilianza na maziwa kwa kuwa saratani ya maziwa ni kubwa zaidi kuliko hatari ya ile ya fuko la uzazi, na operesheni ya fuko la uzazi ni kubwa zaidi," ameandika Jolie.

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 37 amesema kwamba tarehe 27 Aprili alikamilisha miezi mitatu ya taratibu za kitabibu kuhusiana na operesheni hiyo ya kuondosha matiti na kwamba sasa kiwango cha uwezekano wa kupata saratani kimepungua hadi asilimia tano.

Jolie na mumewe, ambaye pia ni muigizaji maarufu, Brad Pitt, wana watoto watatu wa kuwazaa na watatu wa kuwalea, na ameandika kwamba sasa anaweza kuwaambia watoto wake kwamba hawapaswi kuwa na hofu ya kumpoteza mama yao kwa sababu ya saratani.

0 comments:

Post a Comment