Blogger Widgets

Tuesday, May 21, 2013

Makala: Jinsi Nay wa Mitego na Roma walivyoweza kujitengeneza kama wasanii wa biashara

Miongoni mwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo wasanii wa hip hop nchini ni kuingiza fedha kutokana na kazi zao. Bahati mbaya njia pekee na za uhakika za kuingiza fedha kupitia muziki zilizobakia ni malipo ya show na yale yanayotokana na miito ya simu.


page
Ni miaka takriban mitano sasa hakuna tena usambazaji wa albam unaoaminika kama ule wa zamani kwakuwa wasambaji wa muziki wanaonekana kuususia muziki wa Bongo Flava.

Kwakuwa shows na miito ya simu ndio njia pekee zilizobakia kumuingiza fedha msanii wa Tanzania, inahitajika kazi ya ziada kutengeneza nyimbo zinazoweza kuwavutia wadau wanaohusika.

Kwa miaka mingi, wasanii wanaofaidika zaidi ni wale wanaoimba (Ali Kiba, Diamond, Dully Sykes, Ommy Dimpoz na wengine). Watu wengi wameendelea kuamini kuwa Hip hop ni muziki wa kupata heshima tu Tanzania lakini haulipi.

Chukulia mfano wasanii wenye sifa kubwa za kiuandishi kama Nikki Mbishi, One the Incredible, Nash MC na wengi wa aina hiyo kwenye kizazi chao. Rappers hawa licha ya kukubalika kwa uwezo wao usio na kifani, muziki wao umeendelea kubaki kuwapa heshima tu lakini usiowaingizia fedha inayostahili. Lakini hali hii ni tofauti kwa Roma na Nay wa Mitego.

Roma
Jina la Roma lilianza kufahamika kwenye wimbo Mr President na kumtambulisha rapper huyo kwa identity yake ya rap ya ‘kupayuka’ na kama rapper mwenye mrengo wa kimapinduzi zaidi ‘radical rapper.’ Kwa lugha nyingine rahisi, Roma alionekana kama mwanaharakati.

Roma alijitengenezea upekee wake kama rapper anayeukosoa vikali uongozi wa serikali ya chama cha mapinzuzi, CCM. Licha ya Mr President kuwa wimbo wenye style na beat ‘ngumu’ maudhui yake yaliufanya uwe rahisi kuyakuna masikio ya mashabiki yaliyotaka kusikia anachonena. Uwasilishaji wenye Kiswahili rahisi na maneno yanayoeleweka moja kwa moja ni sababu nyingine iliyoupa uhai wimbo huu.

Baadhi ya nyimbo zake zilipata wakati mgumu kupata airtime kwenye vituo vingine vya radio. Baada ya Mr President, Roma aliendelea kutoa nyimbo zenye muelekeo ule ule ukiwemo Pastor uliokuwa ukizungumzia jinsi dini inavyotumika kibiashara na pia Mathematics ambamo alizungumza mengi na kuikosoa serikali na watu binafsi.

Ingawa alikuwa ameshanza kupata mashavu, Mathematics ndio wimbo uliompa mafanikio zaidi.

Mwaka 2011 na mwishoni mwa 2012, Mathematics ilikuwa ni hip hop anthem kwenye kila radio nchini. Umaarufu wa Roma uliongezeka maradufu. Ukubwa wa Mathematics ulidhihirika wazi kwenye tuzo za Kili kwa kuwa wimbo bora wa Hip Hop mwaka 2012.

Pamoja na kufanya hip hop ngumu, Roma amekuwa akipata mashavu kibao ya shows. Ni miongoni mwa wasanii wachache wa hip hop Tanzania wanaojulikana kwa kupiga show nyingi za promotion za makampuni mbalimbali nchi nzima.

Hizi ni baadhi ya sababu zilizomfanya Roma awe msanii wa hip hop wa biashara:

1.Ni kuegemea kwenye utunzi wa nyimbo za kimapinduzi zinazowagusa wananchi wengi hususan vijana waliochoka na jinsi hali ya kiuchumi ilivyo nchini

2. Mashairi yake kuendana na hali halisi ya maisha ya mtaani

3.Ujasiri wake wa kusema mambo kwa uwazi bila kuogopa wahusika anaowataja kwenye nyimbo zake. Ama kwa maana nyingine Roma husema mambo ambayo wengine huogopa kuyasema.

4. Uwezo wake mkubwa wa kulitawala jukwaa wakati wa kuperform kitu kinachosaidiwa na rap yake ya kupayuka ambayo ni nzuri kwenye live performance.

5. Uandishi wa maishari ya kiubunifu yanayoeleweka kwa urahisi. Hatumii sana metaphors kama wana hip hop wengine. Hii ni kwakuwa mashabiki wa kawaida hawapendi kuumiza kichwa kujaribu kuelewa mistari ya wimbo). Pia amekuwa akiepuka matumizi ya mistari ya Kiingereza.

6. Ile hali ya kuonekana kama mwanaharakati.

Nay wa Mitego
Kumekuwepo na mjadala mrefu kuhusiana na kama Nay wa Mitego ni mwanahip hop ama anafanya Bongo Flavour (kwa kuzingatia neno bongo flava linavyotafsiriwa na wengi kama muziki wa kuimba zaidi).
Wadau wengi wa hip hop licha ya Nay kujiweka kama msanii wa hip hop, wanadai kuwa hafanyi hip hop. Mjadala huo tunawaachia mashabiki wanaosikiliza nyimbo zake.

Kama Roma, Nay alianza kwa kujitengeneza kama msanii asiyeogopa kukosoa ama kuponda jambo analohisi haliko sawa. Tofauti na Roma, Nay hakuongelea siasa. Yeye alideal na maisha binafsi ya wasanii wenzie. Kama unakumbuka kwenye Itafahamika, Nay aliwadiss wasanii wengi waliopoteza umaarufu, wakiwemo Inspekta Haroun, Sister P, Rah P, Dudu Baya, P-Funk na wengine.
Aina hiyo ya muziki wake ilimtengenezea maadui wengi hasa wasanii aliowaponda pamoja na mashabiki wao, lakini pia akaanza kujipatia mashabiki wake waliyemuona ni mtu asiyekopesha (asiyeogopa kuongea ukweli).

Mwanzo Nay alichukuliwa kama rapper anayetumia njia ya kudiss wenzie ili kupata ‘cheap publicity’ ama njia ya kupata umaarufu wa haraka. Japo ni ngumu kuthibitisha kama hiyo ndio ilikuwa dhamira yake, Nay ameendelea kuwa msanii wa aina hiyo hiyo. Nyimbo zake nyingi za rap zimekuwa na ujumbe unaoendana na zinazozua mjadala.

Breakthrough yake kibiashara ilichangiwa na ngoma yake ‘Nasema Nao’. Humo aliwadiss watu wengi zaidi. Kauli yake kuwa wasichana wengi wa Bongo Movies ni machangudoa iliwafanya waigizaji wengi wa tasnia hiyo kumuijia juu. Kutokana na wimbo huo, Nay alipata interview nyingi kwenye vituo vya radio na TV vilivyotaka kupata ufafanuzi zaidi wa kile alichokisema. Kuhusu suala la wasanii wa kike wa bongo movie, aliendelea kushikilia msimamo wake na kutoa mifano halisi ya waigizaji aliowashuhudia wakifanya uchangudoa.

Aina ya nyimbo zake, zikamtengenezea mashabiki lukuki nchini.
Mwaka jana alikuwa miongoni mwa wasanii waliozunguka nchi nzima kwenye show za Fiesta. Na huko mara nyingi alikuwa kati ya wana hip hop waliopata shangwe nyingi zaidi. Miaka ya 2012 na 2013 imekuwa na mafanikio makubwa kibiashara kwake. Amefanikiwa kupiga show nyingi zikiwemo za matamasha makubwa na zile za promotion za makampuni hususan ya simu. Nay ameendelea kupata mashavu kwenye promotion zote za Tigo, Vodacom na Airtel ambazo zimemuingizia fedha nyingi.

Mwaka huu amefanikiwa kutengeneza hit single, Muziki Gani aliyomshirikisha Diamond na ambao umemweka kwenye sehemu nzuri zaidi kibiashara.

Hizi ni baadhi ya sababu zilizomfanya Nay awe msanii wa biashara:
1. Kurap masuala ya ukweli yanayowahusu wananchi wengi bila kukwepesha
2. Kukosoa wasanii wanaofanya mambo yasiyopendeza
3. Kuandika mashairi yenye utata (controversial lyrics)
4. Kuandika mashairi rahisi yanayoeleweka kwa urahisi
5. Uwezo wake wa kubadilika kwendana na soko
6. Ujasiri wake na uwezo wake wa kusimama kwenye kile anachokiamini

Uchambuzi umefanywa na Fredrick Bundala (Bongo5 Head of Content).Twitter: @skywizz

0 comments:

Post a Comment