Blogger Widgets

Saturday, February 23, 2013

Yule Shujaa wa Wameru aliyedai ardhi Umoja wa Mataifa huyu, msome



na. Neema Kishebuka:


               

UKIFIKA katika kijiji cha Pori na kutaja jina la Dk. Japhet Kirilo linafahamika kwa watu wa rika zote wa kabila la Wameru kutokana na historia yake enzi za uhai wake katika kutetea maslahi ya watu wa Meru.

Baada ya kufika katika kijiji hicho nikiwa na baadhi ya viongozi kadhaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) tunakutana na Nderetwa Kirilo ambaye ni mke wa Dk. Kirilo na anatukaribisha nyumbani kwake na kuanza kutupa ramani fupi huku akiwa na tabasamu.

“Hapo unapopaona ndipo mahala ambapo alikuwa anakaa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akimtembelea mume wangu wakati wa kudai uhuru toka kwa wakoloni,’’ anaanza kueleza Nderetwa (85) wakati alipotembelewa na wabunge Vicent Nyerere (Musoma Mjini), Mchungaji Islael Natse (Karatu) na viongozi wengine wa CHADEMA wakiongozana na mgombea ubunge wa Arumeru Mashariki kupitia CHADEMA, Joshua Nassari.

Anaanza kueleza historia fupi ya Mzee Kirilo huku akimshika mkono Vicent na kusema, “Baba yako alikuwa mcheshi sana alipenda kunitembelea kila wakati alipokuwa anafika Meru.

Alikuwa anapenda nyama ya kuchoma, alikaa katika chumba hicho na kulala siku zote alipokuwa hapa,” huku akionyesha chumba ambacho kwa sasa amekifanya sebule huku mlangoni kukiwa na picha ya Mwalimu Nyerere.

Anasema Dk. Kirilo alikuwa daktari wa magonjwa ya binadamu na alikuwa rafiki kipenzi wa Mwalimu Nyerere, lakini kutokana na mapenzi yake makuu kwa watu wa kabila la Meru, aliamua kuacha kazi ya kuajiriwa na kupigania haki ya Wameru kwa kudai ardhi iliyokuwa ikishikiliwa na wakoloni.

“Dk. Kirilo alichangiwa pesa na Wameru kwenda kudai ardhi Umoja wa Mataifa, lakini hakufanikiwa kwa kuwa ilionekana Meru haikuwa katika orodha ya mataifa koloni, kwa kuwa haikuwa nchi, akaamua kurudi kuungana na Mwalimu Nyerere kuhakikisha wanawaondoa wakoloni.

“Mwalimu Nyerere alikuwa anafika nyumbani hapa mara kwa mara kuja kupanga mipango ya ukombozi na alikuwa analala hapahapa na nilikuwa nawapikia chakula kabla hawajaelekea katika shughuli zao za ukombozi. Nashukuru Mungu walifanikiwa baada ya miaka kama nane tulipata uhuru, hata alipofariki mume wangu, Mwalimu alihuzunuka mno na alikuja msibani,” anasema.

Anasema kabla ya safari hiyo ya Umoja wa Mataifa, mbele ya nyumba yao waliweka chungu ambapo kila mtu alichangia kiasi chochote cha fedha na zilipopatikana za kutosha alituma kama nauli kwenda Umoja wa Mataifa kudai ardhi ya kabila lake mwaka 1952.

Bibi huyo ambaye ana watoto 10 aliozaa na Dk. Kirilo, anasema mumewe alizaliwa mwaka 1921 na kufariki Mei 30, 1997.

Anasema jina Kirilo ni kubwa katika kabila la Wameru na kutokana na heshima yake, ataendelea kukumbukwa na kuenziwa kwani alipenda kuona kabila hilo halionewi wala kunyanyaswa.

Hata hivyo, anaeleza masikitiko yake kuwa Meru iliyokuwa ikipiganiwa na Kiliro sasa inataka kupoteza maadili yake na kuongeza kuwa hata Mwalimu Nyerere na Kirilo wangeamka leo hii wangeshangaa jinsi ardhi ya Meru ilivyoingiliwa na wageni ambao wamehodhi maeneo makubwa.

“Laiti leo hii Mwalimu Nyerere angeamka na kukuta ardhi yetu walivyopewa wawekezaji kulima maua badala ya mazao sijui ingekuwaje,’’ anasema.

Anasema mfano mzuri ni mashamba yaliyochukuliwa kwa ajili ya kupandwa maua huku Wameru wenyewe wakikosa maeneo ya kulima mazao.

“Wazee waliipigania mno ardhi ya Meru na ndiyo maana waliweza kwenda mbali zaidi kuhakikisha wakoloni wanaachia ardhi yetu, lakini vyote hivyo vimesahaulika kwa sasa,’’ anaeleza kwa masikitiko.

Mbele ya nyumba ya mpigania uhuru huyu ambaye bado ameacha historia kubwa katika kabila hili ndipo lilipo kaburi lake ambapo eneo hilo limezungushiwa uzio na kujengewa ngao kubwa.

Wageni mbalimbali wamekuwa wakifika nyumbani hapo kuzulu kaburi la shujaa huyo aliyekuwa na uchungu wa kuona kabila lake linabaki kuwa huru, ndoto ambayo ilikuwa kweli mwaka 1961.

Leo hii mashujaa hao hawapo imebaki historia ambayo itaendelea kuendelezwa siku hadi siku kwa vizazi vijavyo na uwepo wa kaburi hilo katika kata ya Pori ni moja ya kumbukumbu itakayokumbukwa daima na watu wa kabila la Meru na taifa kwa ujumla.

3 comments:

  1. Tutakukumbuka mno mtetezi wa Meru,R.i.p Mzee Krilo.Miss you father.

    ReplyDelete
  2. Story mzuri sana ila rekebisha hapo mwanzo ni Poli sio Pori
    Kazi mzuri sana
    Historia ya Mzee Kirilo ni yakishujaa sana iliyojaa uzalendo

    ReplyDelete