Blogger Widgets

Wednesday, March 20, 2013

BIBI WA MIAKA 90 ASIMULIA ALIVYOLAWITIWA USIKU KUCHA...

Ajuza wa miaka 90, amedai mahakamani jinsi alivyolawitiwa usiku kucha na kijana wa rika la mjukuu wake baada ya kuvunja mlango na kuingia ndani.  
Kabla ya kutoa ushahidi huo, hivi karibuni Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, ililazimika  kuhamisha kesi  kutoka Mpanda Mjini hadi ofisi ya Serikali ya Kijiji  cha  Bulembo, anakoishi bibi huyo.
Bibi huyo (jina limehifadhiwa), alitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Wilaya ya Mpanda, Chiganga Tengwe, akiwa  amekaa  kwenye  mkeka,  kutokana na  umri mkubwa lakini pia matatizo ya kupooza  viungo.  
Akiwa  shahidi wa tatu kati ya wanne waliotoa ushahidi wao, bibi huyo alidai kwamba usiku  wa Desemba 22 mwaka  jana, mshitakiwa Sindebula Msangi (32), alivunja nyumba yake  na kumwingilia  kwa nguvu kinyume cha maumbile.
“Bahati mbaya sana mimi naishi pekee yangu, hivyo usiku  huo mshitakiwa alivunja mlango wa nyumba yangu, akanishika kwa nguvu. Nilimsihi hivi unanifanyia hivi,  mbona kuna mabinti  wengi mtaani?
“Lakini alikaidi na kutimiza azma yake akaniingilia  kinyume  cha maumbile na kunijeruhi na kunisababishia  maumivu makali,“ alidai.
Alidai kuwa usiku huo, mshitakiwa aliendelea kumlawiti mara kadhaa, mpaka alipochoka na kusinzia chumbani humo baada ya kupitiwa na usingizi mzito.
Kwa mujibu wa bibi huyo, ilipofika  saa 12 asubuhi, mshitakiwa akiwa amelala fofofo, alifungua dirisha  la chumba na kumwita mpitanjia aliyemtambua kwa jina la Ashabola Elly.
Alidai alimwita Ashabola kwa ishara ya vidole akaja na kuingia chumbani ambamo alimkuta mshitakiwa amelala fofofo.
Bibi huyo alidai kuwa Ashabola alinyata na kutoka nje ya  nyumba hiyo, bila kumwamsha mshitakiwa huyo na kutoa taarifa kwa majirani na uongozi wa kijiji hicho.
Hata hivyo, kwa mujibu wa bibi huyo, majirani na viongozi hao walipofika  nyumbani hapo mshitakiwa alikuwa tayari ameamka na kutokomea kusikojulikana kwa muda, hadi alipokamatwa baadaye.
Kwa mujibu  wa  hati ya mashitaka, mshitakiwa anadaiwa  kutenda kosa hilo Desemba 22 mwaka jana saa nane  usiku kijijini Bulembo, katika kambi  ya wakimbizi  ya Katumba.
Mshitakiwa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 28 mwaka jana.
Hata hivyo alikana mashitaka na Hakimu Tengwe aliamuru mshitakiwa arudishwe rumande hadi Machi 28, atakapojitetea.

0 comments:

Post a Comment