Blogger Widgets

Tuesday, March 12, 2013

Dada zetu wanavyoandaliwa kuwa malaya wa Ulaya!

 
HAYA mkorofi wangu utasema nini sasa? Si umesikia? Wanaoleta fujo ni wale wanaoandamana kwa amani si wale wanaoua katika kuzuia maandamano ya amani. Wewe haumo? Haya na wenye kukemewa ni wale wanaojaribu kufichua uozo uko wapi si wale wanaotumia nguvu za kila aina kuzuia ukweli usijitokeze. Wewe hujapaza sauti kihivyo?

Yaani mpenzi, ungejua mnavyolaaniwa na walio nacho nadhani masikio yenu yangebaki majivu kutokana na kuwaka moto. Narudia kusema mpenzi, hakikisha kwamba unavaa kofia yako ya bodaboda kila wakati, maana hizi risasi hazina kosa bali nyinyi wenye vichwa vigumu vya kukaribisha risasi ndio wakosaji wakubwa.

Ndipo hapo nashangaa mpenzi. Kila siku wakati wa taarifa ya habari asubuhi na jioni napenda kuibiaibia na ingawa sielewi sana hii lugha ya wenyewe bado naona. Naona watu wanaandamana kwa nguvu sana katika nchi mbalimbali lakini mwisho wa siku kuna mapatano fulani na wanapata haki zaidi. Hata walimu wa Kenya wamekubaliwa. Niliona kweli polisi wameua sana huko Afrika ya Kusini lakini ilibidi Rais aombe radhi na tume iundwe haraka sana maana ilionekana aibu kubwa sana ya kitaifa.

Iweje walinzi wa amani waue? Hata kama watu wamegoma na kuandamana kwa nguvu, walijua kazi ya polisi ni kulinda amani, si kuua amani. Na huko Kenya tena nilifurahi maana jamaa alikuwa anamwaga Kiswahili kuelezea jinsi mgomo ni haki ya kila mfanyakazi anapoona kwamba jitihada zake zote kupata haki zimegonga mwamba. Iweje Wabongo tu ni wakorofi wanapoona kwamba na wao wanahitaji kutetea haki zao?

Lakini kama kawaida yangu, Hidaya wako anakula pini hadi anaogopa itamtoboa tumbo lake. Nabaki namshabikia Binti Bosi anapocharuka na pamoja na baadhi ya wageni wa Bosi wenye mawazo tofauti kidogo. Yaani nacheka kila siku kuona uso wa Bosi unavyogeuka rangi ya mkaa anapopingwa. Bosi hana simile nakuambia, hawezi kuficha hasira zake, sijui alikuwa mbabe wa namna gani alipokuwa kijana. Au ni kawaida ya mabosi kuzoea kupapatikiwa na hata kupakatwa kiasi kwamba mwingine akipinga anaonekana msaliti wa mwisho.

Aaaah! Niache mambo hayo maana ni yaleyale kila siku … labda mkaa uwake moto pia. Uliona ile habari ya Mbeya mpenzi? Ya msichana wa miaka 12 kuswagwa danguroni? Tena kaswagwa huko na mke wa mlinzi wa taifa? Yaani … nikimfikiria mdogo wako wa miaka 12 sipati picha kabisa. Utapelekaje katoto kadogo namna hiyo danguroni? Kuna siri gani imefichika hapa?

Tena kilichonishtua zaidi mpenzi ni kwamba yule msichana akasema eti wanaandaliwa kwenda Ulaya. Dada zangu wanaandaliwa kuwa malaya wa Ulaya! Hapo nilishindwa kujizuia ikabidi nimwulize Binti Bosi. Kumbe yeye alikuwa hajaona hii stori ikabidi asome kwanza kisha akagonga meza kwa nguvu.

‘Yaani Hidaya, hii ni mbaya sana. Unajua watu wakipelekwa huko ni kama watumwa. Waliowapeleka huko wanawafungia ndani na msichana akileta ubishi wa aina yoyote anapigwa na kubakwa na kubakwa na kubakwa hadi anakoma na kukubali chochote. Hivi sisi kweli tumefikia hali hiyo ndani ya nchi yetu?’

‘Sijui dada lakini si unaona stori yenyewe.’

‘Mmmh, haiwezekani! Hivi wanaharakati wako wapi katika hilo? Dada zetu wanauzwa hivihivi hakuna hatua yoyote? Ngoja.’

Nilijua maana ya ‘ngoja’ ile hivyo niliandaa kofia yangu ya bodaboda mapema. Bosi alipofika mezani usiku akakuta gazeti limefunguliwa vizuri ili aone stori hiyo. Akasoma.

‘Asante kwa kunipa hiyo. Kweli huyu msichana ametendewa vibaya sana lakini si unaona aliyemtendea hivyo ameadhibiwa.’

‘Msichana mwenyewe hajaridhika. Na marafiki zake katika biashara ile wakimchangia faini, atakuwa amepata adhabu gani? Hata kwenda jela hakuna.’

‘Lakini angalau ameaibishwa.’

‘Baba, watu kama hawa wana aibu kweli? Iwapo wako tayari kuuza binadamu wenzao, tena watoto, tena hata ndugu zao, wataona aibu mbele ya nani? Shetani? Watu kama hao wanapaswa kufungwa kwenye jela maalumu ambako wakishafungwa, ufunguo wa kufuli unatupwa baharini wasionekane tena.’

‘Ohoo umeanza mihemko yako. Mimi nilidhani unahubiria utawala wa sheria.’

‘Iwapo sheria zenyewe ni za haki, sawa, lakini iwapo sheria inalinda uhalifu, basi utaliwa na sheria badala ya utawala wa sheria. Tena naona hukusoma hadi mwisho.’

‘Nilisoma.’

‘Sasa kuadhibiwa kwa yule kunatosha? Je, wale 10 waliosafirishwa kwenda Urusi? Walisafirishwaje? Walipataje pasi ya kusafiria? Lazima hii ni biashara kubwa kama ile ya kuwapitisha wahamiaji haramu nchini kwetu?’

‘Una ushahidi gani?’

‘Soma hiyo stori baba! Kwani hawa wasichana 10 ni wa kwanza? Na kama biashara hii inafanyika huko Mbeya unafikiri haifanyiki miji mingine? Kweli wewe unapenda kuwa waziri katika nchi inayofumbia macho utumwa wa kisasa?’

‘Ohooo, yaleyale. Yaani mimi siwezi hata kula chakula changu kwa amani baada ya kufanya kazi ngumu siku nzima. Kwa nini usifanye kama wale watoto wehu wa Waziri mwenzangu na kujiunga na wakorofi hadharani ili niabike na mimi?’

BB akashusha pumzi kwa nguvu na kukaa kimya kwa muda. Bosi alifurahi na kuanza kushambulia msosi wake. Lakini baada ya muda BB alisema kwa sauti laini.

‘Lakini baba hujajibu maswali yangu.’

‘Nitajibuje?

Kwani mimi ni bosi wa Uhamiaji au Ustawi ya Jamii? Waache watu wafanye kazi zao.’

‘Mimi ningependa kusikia kutoka kwako kwamba serikali yako imeshtushwa sana na habari hizo na mikakati maalumu inapangwa kukomesha mtu yeyote anayetaka kurudisha enzi za utumwa.’

‘Kwani lazima kila kitu kitangazwe hadharani? Unajuaje kama hatua hazichukuliwi?’

‘Niambie basi baba. Maana ninachoona ni mipango maalumu eti ya kuwakamata wasichana ambao wanafanya ukahaba. Si ajabu baadhi yao walitekwa hivihivi kama huyu msichana au kulazimishwa kwa namna moja au nyingine. Kwa nini pasiwe na operesheni maalumu ya kuwakamata wanaoendesha biashara ya kuwageuza hawa wasichana makahaba? Au kwa kuwa ni wakubwa?’

‘Wakubwa gani? Kwani huyu ambaye amehukumiwa kifungo ni mkubwa?’

‘Inawezekana anaungwa mkono na wakubwa’

‘Ushahidi uko wapi?’

‘Ushahidi ni kwamba wasichana wanatoroshwa hapa nchini bila hata hatua kuchukuliwa. Haiwezekani wasichana wapitishwe hivi kuelekea Urusi au wapi sijui bila wahusika kushtuka?’

Kumbe Bosi siku ile alikuwa ameacha mkaa mahali pengine au kwa kuwa haikuhusisha malumbano ya vyama, aliamua kukubali yaishe.

‘Haya mwanangu, nitawauliza wahusika kesho wanafanya nini katika mambo hayo. Sawa? Na nitakuambia.’

BB alitabasamu kwa nguvu.

‘Asante sana baba.’

Bosi naye akatabasamu na kuelekeza nguvu zake zote katika kutafuna. Lakini BB hana dogo nakuambia. Akamwacha baba yake kwa muda kidogo kisha akasema.

‘Samahani baba, sichokozi zaidi lakini kweli nataka kujua. Kwa nini hawa wanasemwa eti wanauza miili yao. Hivi ukiuza kitu unabaki nacho? Sasa kama wameuza miili tayari, wamebaki na nini? Na kama unaweza kuuza kitu na kubaki nacho, vibarua nao hawauzi mikono yao na miguu yao? Kwa nini hatusemi kwamba wanauza miili yao pia? Na wasomi hawauzi vichwa vyao?’

Mama Bosi alitaka kuingilia kati.

‘Wewe mwananangu, na wewe huoni aibu kuongelea hayo ….’

Lakini Bosi akacheka kwa nguvu sana hadi alimwaga vipandevipande vilivyokuwa mdomoni mwake.

‘Lo, mwanangu sikuwezi kabisa. Tuseme nini basi, wanauza ngono?’

Akaondoka huku akicheka sana. Lakini mpenzi huoni hali hii? Vipi huko kwetu? Wadogo zetu hawauzwi hivyo? Kwa nini biashara hii ya utumwa inaendelea kimyakimya? Kwa nini hakuna anayeshtuka?
  
Chanzo: Raia Mwema - Dada zangu wanaandaliwa kuwa malaya wa Ulaya!

0 comments:

Post a Comment