Blogger Widgets

Monday, March 4, 2013

Mieleka ya asili inavyovutia vijana

 
 

MCHEZO wa mieleka ni mchezo unaohitaji nguvu na huchezwa sehemu mbalimbali duniani kwa kanuni na sheria tofauti.
Ipo mieleka inayochezwa kisasa ambayo imeingiza michezo mingine ya kupigana, lakini ipo mieleka ya asili ambayo haihusishi aina nyingine za kupigana.
Kati ya michezo hiyo ya mieleka ya asili upo mchezo wa mieleka wa asili wa Senegal.
Mchezo wa mieleka nchini Senegal kwa asili ulianzia kwa watu Serer, lakini baadaye mchezo huo ulikuwa maarufu na kuwa mchezo wa taifa wa Senegal, pia katika nchi ya Gambia.
Kwa raia wa Senegal, mchezo huu wa mieleka wanauita kwa jina la kwao ambalo ni Laamb.
Kihistoria mchezo wa mieleka nchini Senegal ulianzia kwa watu wa Serer ambao walikuwa wakiutumia kama sehemu ya mazoezi kabla ya kwenda vitani, pia ulikuwa ikitumiwa na wavuvi baada ya kazi zao, lakini baadaye mchezo huu ukawa unatumiwa na vijana kuonyeshana uwezo wao wa nguvu, kupata wake, kuthibitisha uanaume wao au kuleta heshima kijijini, ambapo mvuto wake ukaufanya kuwa mchezo wa mashindano.
Katika karne ya 14 baada ya mchezo huo kuwa wa kimashindano, aliibuka bingwa Boukar Djilak Faye kutoka kwa watu wa Serer ambaye alishinda mapambano mengi na kuwa mtu maaarufu katika nchi za Senegal na Gambia.
Tangu miaka ya 1950 mchezo huu wa mieleka ya asili nchini Senegal ulikuwa kwa kasi zaidi kimashindano na kupata watazamaji wengi na kuwa kivutio cha utamaduni kwani pia zawadi za fedha zilianza kutumika katika kipindi hiki.
Hivi sasa mchezo huu nchini Senegal unaendeshwa kibiashara na mapromota ambao wanatoa zawadi za fedha nyingi kwa washindi na ushindani wake umekuwa mkubwa zaidi.
Kutokana na hali hiyo, wacheza mieleka nchini Senegal wanafanya sana mazoezi tofauti, magumu kwa ajili ya kujiongezea nguvu, pia wacheza mieleka hao wanatumia madawa ya kienyeji kabla ya mapambano yao wakiwa na imani yanawaongezea nafasi zaidi ya ushindi.
Mabingwa wa mieleka wanaofahamika sana nchini Senegal ni Yekini (Yakhya Diop), Tyson (Mohamed Ndao) na Bombardier (Serigne Ousmane Dia).
Mapromota wa mchezo wa mieleka nchini Senegal wanautangaza mchezo huu na wadhamini wamejiingiza sana kiasi kwamba yapo mapambano mjini Dakar ambayo bingwa huchukua kitita za dola 120,000 au zaidi ya hapo kwani wapo mapromota ambao hutumia kiasi cha dola 400,000 kuandaa pambano moja kubwa.

0 comments:

Post a Comment